Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amewataka wadau wa Misitu kutumia ubunifu kuwajengea uwezo Wananchi namna ya kuongeza thamani mazao ya Misitu kunufaika na fursa za kiuchumi zitokanazo na sekta hiyo kuwa na urahisi kwenye utunzaji wake.
Ameyasema hayo akiwa Wilayani Same wakati akitembelea mabanda ya Maonesho kwenye kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Same kunakofanyika maadhimisho siku ya Misitu na Upandaji Miti yanayofanyika kitaifa mkoani humo akiwataka wananchi hasa wakazi wa Same kushiriki maadhimisho hayo kupata ujuzi wa namna ya kunufaika kupitia sekta hiyo.
“Niwapongeze Wadau wote mliojitokeza kutoa elimu kuhusu uhifadhi na utunzaji wa misitu hii inasaidia kupanua wigo wa uelewa kwa wananchi juu ya namna wanaweza kunufaika kupitia sekta hiyo hali ambayo itasaidia uelewa wa umuhimu wa kutunza mazingira kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi”. Alisema Waziri Kairuki.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa huduma za Misitu nchini Prof. Dos Santos Silayo amesema maadhimisho hayo pamoja na mambo mengine yanatumika kutoa elimu hasa ya masuala ya uhifadhi, msisitizo ukiwa kwenye kupanda miti kwenye maeneo ambayo yanausimamizi ikiwemo ya hifadhi na taasisi nyingine za Umma.
Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amesema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 zaidi ya Miti Milioni 1.7 imekwisha pandwa kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo akisema kufanyika kwa maadhimisho ya siku ya Misitu na Upandaji miti kitaifa kutasaidia kuongeza hamasa zaidi mpango wa sasa ni kuongeza umakini kwenye usimamizi kuhakikisha miti iliyopandwa inakua.
Maadhimisho ya Siku ya Misitu na Upandaji Miti Duniani yatafikia kilele chake Machi 21, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akitarajiwa kuwa Mgeni rasmi siku hiyo.
0 Comments