NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
SHIRIKA la Umeme nchini Tanesco mkoa wa Kilimanjaro limeanzisha huduma maalum ya Mobile clinic yenye lengo la kuwafuata Wateja wake na kusikiliza kero zinazowakabili katika sekta umeme na kuzipatia ufumbuzi papo hapo.
Hayo yalibainishwa jana na Afisa Uhusiano huduma kwa wateja Tanesco mkoa wa Kilimanjaro, Mwanaisha Mbita ambapo alisema kuwa, kupitia huduma hiyo watumishi wa shirika hilo watatembelea kata kwa kata ili kutatua kero na kurahisisha huduma.
Mwanaisha alisema kuwa, wateja wengi wa huduma hiyo wanapatikana vijijini ambapo imekuwa ikiwawia vigumu kufika katika ofisi za shirika hivyo wameamua kurahisisha huduma kwa kuwafuata wateja katika maeneo ya makazi yao.
“kwa wale wateja wetu ambao wanakero mbalimbali lakini wanashindwa kufika ofisini sasa ni wakati wao tumeamua kutoka ofisini na kuja kuwafikia ili kuzitatua kero zinazowakabili papo hapo lengo ni kuhakikisha Wateja watu wanapata huduma bora na ya uhakika.
Alisema kuwa, siku ya kwanza ya uzinduzi wameweza kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wateja 120 hali ambayo imeonyesha huduma hiyo kupokelewa kwa muamko mkubwa na kudai kuwa itakuwa ni endelevu.
Afisa Uhusiano huyo alisema kuwa, kuanzishwa kwa huduma hiyo itawasaidia Wateja kupunguza gharama zao pamoja na muda kufika ofisi za Tanesco kwani watapata ufumbuzi wa matatizo yao papo hapo.
Alisema kuwa, wapo baadhi ya wateja wapya ambao wamekuwa wakitaka kufungiwa umeme kupitia huduma hiyo mteja atalazimika kulipa na kufungiwa umeme kwa haraka zaidi.
Aidha alitoa wito kwa Wateja wa tanesco kujitokeza kwa wingi pindi wanapoona Watumishi wa Tanesco wamefika katika maeneo yao kutoa huduma ya Mobile clinic.
Kwa upande wake, Antonia Mushi mkazi wa kata ya Karanga manispaa ya Moshi alisema kuwa, huduma ambayo wameianzisha Tanesco ya kuwafikia wateja wake ni huduma nzuri ambayo itamaliza malalamiko ya wateja wengi.
Alisema kuwa, Mobile clinic ni huduma ambayo itawasaidia wateja kupata ufumbuzi kwani wamekuwa na shida mbalimbali lakini hawajui wafanyeje lakini kupitai huduma hii itawakutanisha na wataalam mbalimbali kutoka Tanesco.
Mwisho….
0 Comments