Header Ads Widget

MAELEKEZO KUHUSU WANAFUNZI AMBAO HAWAKUFIKIA ALAMA ZA UFAULU KATIKA UPIMAJI WA KITAIFA WA KIDATO CHA PILI 2025




Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilifanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na kupata Toleo la Mwaka 2023 na mitaala iliyoboreshwa. 

Utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa kwa Mkondo wa Elimu ya Jumla ulianza mwaka 2025 kwa wanafunzi wote wa Kidato cha Kwanza. 

Kwa upande wa Mkondo wa Elimu ya Amali, utekelezaji wake ulianza mwaka 2024 kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza ambapo walifanya Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili mwaka 2025.

Baraza la Mitihani la Tanzania limetangaza Matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili tarehe 10 Januari 2026. Utaratibu uliokuwepo ni kuwa wanafunzi ambao hawakufikia kiwango cha ufaulu unaotakiwa hukariri kidato husika.

Hata hivyo, ninaelekeza kwamba wanafunzi ambao hawakufikia alama za ufaulu za Kidato cha Pili mwaka 2025 waendelee na Kidato cha Tatu mwaka 2026 badala ya kukariri (kurudia) Kidato cha Pili. 

Wanafunzi hao watapewa programu maalum rekebishi (remedial programme) itakayotolewa wakati wakiendelea na masomo yao ya Kidato cha Tatu.

Uamuzi huu unazingatia kwamba mitaala iliyoboreshwa inatekelezwa kwa awamu Wanafunzi waliofanya Upimaji wa Kidato cha Pili mwaka 2025 walitumia mtaala wa zamani na watamaliza Kidato cha Nne kwa kutumia mtaala huo wa zamani. 

Wanafunzi wanaoingia Kidato cha Pili mwaka 2026 watatumia Mtaala Ulioboreshwa ambao walianza kuutumia Kidato cha Kwanza. 

Hivyo, endapo wanafunzi walioshindwa kufikia alama za ufaulu watarudia Kidato cha Pili mwaka 2026.

watalazimika kutumia Mtaala Ulioboreshwa ambao hawakuanza nao Kidato cha Kwanza. Hii italeta changamoto kubwa katika ujifunzaji na ufundishaji.

Maelekezo haya yanawahusu wanafunzi wa Kidato cha Pili kwa mwaka 2025 waliopimwa kwa kutumia mtaala wa zamani. Wanafunzi wa Mkondo wa Elimu ya Amali walioshindwa kufikia alama za ufaulu wataendelea na utaratibu wa kukariri (kurudia) Kidato cha Pili katika mwaka 2026; hii ni kwa sababu wao walianza kutumia Mtaala Ulioboreshwa tangu Kidato cha Kwanza.

Ni matarajio yetu kuwa wakuu wa shule zenye wanafunzi husika watatekeleza maelekezo haya kwa ukamilifu na kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanafundishwa na kujifunza ipasavyo ili kupata umahiri uliokusudiwa.

Dkt. Lyabwene M. Mtahabwa KAMISHNA WA ELIMU

KARIBU JIUNGE NA SHULE BORA ZA ST DOMIC SAVIO IRINGA BOFYA HAPA

JIUNGE NA SHULE BORA YA THE GLORY PRIMARY SCHOOL IRINGA BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI