Header Ads Widget

IJUE SHERIA YA MAKOSA YA KIMTANDAO NA ADHABU YAKE

 


Maendeleo ya teknolojia yanafanya uendeshaji wa biashara sasa uweze kufanyika kwa njia ya mitandao. Nina maana mtu anaweza akauza na kununua bidhaa kwa kutumia mtandao na vilevile kutangaza biashara yake pia kupitia njia hiyo.

Mfano mashirika ya ndege, benki, wajasiriamali pamoja na mashirika yote ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, yanaweza kuendesha biashara zao na kutoa huduma zao kwa kutumia mtandao.

Hivyo basi, bunge la Tanzania limeamua kutunga sheria inayosimamia mambo ya mitandao. Sheria hiyo, ijulikanayo kama Sheria ya Uhalifu wa Mitandao ya 2015, ilianza kutumika mwanzoni mwa mwezi huu.

Sheria hii ina umuhimu mkubwa kwa sababu ya ongezeko la uhalifu wa aina mbalimbali mitandaoni. Sheria hii ilitungwa ili kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Imeweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.

Sehemu ya pili ya sheria hii inaainisha makosa na adhabu dhidi ya makosa hayo ndani ya sheria hiyo; kifungu cha nne kinaelezea kosa la mtu kuingia au kusababishwa kuingiliwa katika mfumo wa kompyuta kinyume na sheria na kutoa adhabu yake ambayo ni kuwajibika kulipa faini ya Sh3 milioni au mara tatu ya thamani ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria, au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote. Baadhi ya makosa mengine yalioainishwa na sheria hiyo ni kama kuingilia takwimu za mawasiliano na utendaji kazi wa mfumo wa kompyuta kinyume na sheria.


Katika masuala ya mitandao kuna mambo mengi ambayo yanaweza kutokea, kwa maana hakuna mipaka. Hivyo, ni vyema suala la busara kuwa na sheria ambayo itasimamia mambo yote yanayohusiana na mitandao pamoja na watumiaji wa mitandao.

Katika uendeshaji wa biashara kuna mambo mengi mazuri na mabaya yanayoweza kujitokeza kwa namna moja ama nyingine, ikiwamo wizi, udanganyifu pamoja na udhalilishaji.

Hivyo basi, sheria hii imejaribu kulinda haki bunifu za wasanii na wafanyabiashara na kuweka adhabu kwa yeyote atakayekiuka na haki bunifu zinazolindwa kisheria chini ya kifungu 24 (b).

Vilevile sheria hii inawalinda wadau wote, wakiwemo wafanyabiashara dhidi ya usambazaji wa taarifa za uongo au taarifa zozote bila idhini ya mhusika. Umuhimu wake unakuja pale ambapo wapinzani wa kibiashara wakianza kuchafuliana sifa kwa ajili ya kuvutia wateja.

Vilevile, ukiangalia makosa yanayohusiana na utambuzi, ambapo mtu au watu wanajitambulisha kwa majina ya uongo au kujifanya kuwa mtua ambaye unamtambua. Anaweza kutokea mtu anayejaribu kufanya biashara yake kwa kujitambulisha na kujifanya kama mtu mwingine mbele ya wateja. Kosa hili la udanganyifu linatendeka sana kwa maana si rahisi kumshtukia mtu kama anasema ukweli au la.

Umuhimu wa sheria hii kibiashara pia unaweza ukaonekana pale ambapo sheria imejaribu kuwalinda watumiaji wa mitandao dhidi ya mashambulizi ya mfumo wa kompyuta, ambazo zinaweza kusababisha upotezaji wa takwimu na kusababisha hasara kibiashara kwa namna moja ama nyingine. Hii hujitokeza pale ambapo wahalifu wanajaribu kuteka nyaraka kwa manufaa yao wenyewe.

Sheria ya mitandao ni muhimu kwetu endapo tutaitekeleza kikamilifu na kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya ulinzi wa biashara zetu.


MAMBO 10 MUHIMU ILI SHERIA YA MAKOSA YA KIMTANDAO YASIKUKAMATE

Sheria ya mitandao iliyoaanza kutumika rasmi tarehe 1 septemba 2015. 

 

  •  Epuka Kusambaza ujumbe wa uchochezi ama ushawishi wa kisiasa unaoweza kuleta athari kwa jamii yetu kupitia mitandao


  •  Epuka Kusambaza au kutunga ujumbe unaoleta uchochezi wa kidini unaoweza kupelekea kuvuruga amani na maelewano kwa jamii kupitia mitandao


  • Epuka Kusambaza picha ama video za utupu ama zilizokosa maadili kwa jamii kupitia mitandao mbalimbali ( Whatsapp, Facebook, YouTube, Instagram n.k)


  • Epuka Kusambaza picha ama video za uchochezi wa kidini ama kisiasa kupitia makundi mbalimbali ama mitandao ya kijamii


  • Epuka Kushiriki kusambaza chochote kati ya vilivyotajwa hapo juu (kutuma kama ulivyopokea ) itakugharimu


  • Epuka Wizi kupitia mitandao mbalimbali na mitandao ya simu utakugharimu


  • Epuka Kumpatia mtu line yako ya simu na kutumika kufanyia wizi ama utapeli itakugharimu


  • Epuka Kushiriki kumchafua mtu,taasisi,kikundi cha watu kwa namna yoyote kupitia mitandao pia itakugharimu


  • Epuka Kupoteza simu bila kutoa taarifa na kufunga mawasiliano hayo yanaweza kupelekea kutumika kufanya uhalifu na ukaangukia hatarini


  • Epuka Kutumia mtandao kwa utapeli kupitia 'brand' ama jina la mtu itakugharimu


Hukumu

Ni kifungo cha miaka kadhaa gerezani ama faini ya fedha isiyopungua milioni 5 kulingana na kosa lililofanyika (au vyote!)


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI