Header Ads Widget

SARE ZA POLISI ZAMTIA MATATANI

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

POLISI mkoani Kigoma wamemtia mbaroni mtu mmoja mkazi wa mtaa Burega manispaa ya Kigoma Ujiji akiwa na sare za jeshi la polisi akizitumia sare hizo kinyume cha sheria.

 

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari mjini Kigoma alisema kuwa mtu huyo ambaye kwa sasa jina lake limehifadhiwa alikamatwa katika operesheni ya kudhibiti uhalifu iliyokuwa ikiendeshwa na polisi mkoani Kigoma.

 

Kamanda Makungu alisema kuwa mtu huyo ambaye kitaaluma ni dereva alikamatwa na sare hizo kombati mbili na suruali mbili (Green Jungle) na kofia mbili zenye nembo ya polisi katika upekuzi uliofanywa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.

 

Akieleza kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo Kamanda Makungu alisema kuwa polisi walikuwa kwenye operesheni ya kuzuia uhalifu na hivyo wakawa wanaendsha msako na kukamatwa watuhumiwa mbalimbali ambapo mtuhumiwa huyo alikamatwa kwa tuhuma nyingine hivyo polisi Kwenda naye nyumbani kwake kufanya upekuzi na ndipo walipozikuta sare hizo.

 

Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa bado haijafahamika mtuhumiwa alikuwa anatumia sare hizo zenye cheo cha Mkaguzi wa polisi kwa minajili gani lakini kutokana na kukamatwa kwa tuhuma nyingine za uhalifu ni wazi mtuhumiwa alikuwa anatumia sare hizo kwa matumizi yasiyo sahihi.

 

Alisema kuwa uchunguzi unaonyesha kuwa hizo siyo sare rasmi za polisi kutokana na jinsi zilivyo shonwa lakini inaonyesha fundi ana uhusiano na polisi kutokana na kushonwa kwa ustadi mkubwa na kwamba kwa sasa mtuhumiwa anashikiliwa kituo kikuu cha polisi mkoa Kigoma.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI