Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amewataka wawekezaji katika sekta ya uchukuzi kutoka nchi ya Japani kwenda kuwekeza nchini Tanzania kwenye miradi ya kimkakati ikiwemo maeneo ya bandari na reli ambayo yana manufaa kwa nchi zote.
Wito huo ameutoa jijini Dar es Salaam wakati alipokua akifungua mkutano wa kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta ya uchukuzi ambapo wamekutana wadau mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Miundombinu ya Japani Afrika (JAIDA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Amesema kuwa, mahusiano kati ya sekta binafsi na Serikali (PPP) yameendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora ikiwemo utendaji wa bandari hapa nchini na kuwavutia wawekezaji toka sehemu mbalimbali duniani.
Aidha, ametaja maeneo yanayohitaji uwekezaji kuwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kuhifadhi makasha katika bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa barabara ya reli ya Isaka-Lusumo-Kigali yenye urefu wa kilomita 495.
Sambamba na hayo amesema sababu zilizopelekea kuongeza kwa Meli Tanzania ni pamoja na uwezeshaji toka serikalini, ongezeko la kina cha lango la Bandari hadi mita 15.5 ambacho kinatosha kuhudumia Meli gatini.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafiri na Utalii kutoka Serikali ya Japan, Mhe. Konosuke Kokuba, amesema kuwa wataendelea kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo kwa kuendelea kujenga miundombinu yenye ubora katika miradi yote inayoendelea na ile ambayo inatarajiwa kutekelezwa.
Amesema kuwa, kutokana ongezeko la watu katika nchi zinazokuwa zinahitaji teknolojia za kisasa katika ujenzi wa miundombinu nchini ili ziweze kutosheleza mahitaji.
Haya yanajiri ikiwa ni siku chache tu zilizopita ambapo Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa alitembelea Bandari ya Dar es Salaam kuendeleza uhusiano wa kibiashara baina ya nchi yake na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania – TPA.
🔴MATANGAZO YA MASOMO CHINI
0 Comments