Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Jumla ya wanafunzi 11970 kati ya wanafunzi 21326 waliojiandikisha sawa na asilimia 56.1 hawajaripoti shule za sekondari walizopangiwa hadi sasa katika mkoa wa Njombe licha ya serikali kuondoa masharti magumu ikiwemo wanaokosa sare na vifaa vingine.
Ripoti hiyo imetolewa na Ofisa elimu mkoa wa Njombe Mwalimu Nelasi Mulungu wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa kutembelea shule mbalimbali kukagua hali ya wanafunzi kuripoti shule.
Baada ya kutembelea shule za Sekondari Lunyanywi na Mpechi sekondari mjini Njombe Mwalimu Mulungu amesema hadi januari 15 mwaka huu jumla ya wanafunzi 9356 pekee sawa na asilimia 43.9 ndio walioripoti shule jambo ambalo hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa.
Mwalimu Brown Kiswaga ni mkuu wa shule ya sekondari Mpechi ambaye amesema shule hiyo kwa sasa haina changamoto yoyote hivyo anawaomba wazazi kuwapeleka shule watoto waliopangiwa hapo.
Hata hivyo mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe Kuruthum Sadick amesema hakuna mtoto atakaye achwa nyumbani ilihali amefaulu hivyo hatua kali zitachukuliwa kwa wazazi watakaoshindwa kuwapeleka wanafunzi shule.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka amesema hakuna sababu ya mzazi kutompeleka shule mtoto ilihali ameondoa vikwazo vingi.
Baadhi ya wazazi akiwemo Magnus Mlowe ambao wameshawapeleka watoto shule wameitaka jamii kutambua umuhimu wa elimu huku Mwanafunzi Warid Danda akiwaasa wanafunzi wenzake kuzingatia masomo.
0 Comments