Na Hamida Ramadhan Matukio, APP Dodoma
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) Deus Sangu amesema Muswada wa Uwekezaji wa Umma unatarajia kupelekwa bungeni na endapo ukipitishwa utaanzisha Taasisi ya Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania ambayo itachukua majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo itafutwa.
Mwenyekiti huyo amebainisha hayo bungeni jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha zoezi la kupokea maoni ya wadau kuhusu sheria hiyo.
Amesema lengo la muswada huo ni kufanya marekebisho makubwa kwenye ofisi ya msajili wa hazina ambayo ilikuwa na majukumu ya kusimamia mashirika ya umma
“Tangu kuanzishwa kwa ofisi ya msajili wa hazina kumekuwa na ombwe kwenye uendeshaji wa mashirika ya umma. Endapo Bunge litaridhia kupitisha muswada huo tutafuta Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania ambayo itakuwa na dhima kusimamia kwa ukaribu mashirika ya umma,”amesema
Sangu amesema kwa mujibu wa takwimu hadi kufikia Juni mwaka jana kulikuwa na mashirika ya umma 304 ingawa tija inayokusudiwa bado imekuwa iko chini
Amrsema serikali imewekeza zaidi ya sh.trilioni 76.7 katika mashirika hayo ambapo fedha hizo ni bajeti ya miaka miwili ya nchi.
“Lengo la serikali kuwekeza fedha hizo ni kuona uwekezaji unakuwa na tija katika maeneo mbalimbali pamoja na kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwasababu serikali ndio muwekezaji mkubwa,”amesema.
Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela (CCM) amesema baada ya muswada huo kupitishwa utaanzisha Mfuko wa Uwekezaji ambapo itahakikisha mashirika yote yanakuwa na mitaji ya kutosha kwa ajili ya kujiendesha.
“Tumepokea maoni ya wadau zaidi ya 50 na tunaendelea kupokea kupitia ofisi ya Bunge baada ya hapo kamati itakaa kwa ajili ya kuyachakata na kuwasilisha ndani ya bunge ili kuridhia kuwa sheria kamili ambayo itaanzisha taasisi mpya.
Ameongeza kuwa :”Tunaamini sheria hii ikipita kutakuwa na mambo mazuri ikiwemo wakurugenzi wa bodi za taasisi kutewuliwa kwa njia ya ushindani ambapo na wale wenye sifa ndio watapata nafasi.
Katika hatua nyingine wadau wamempo Rais Samia kwa kwa kufungua uwekezaji .
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau waliofika kwa ajili ya kutoa maoni wamempongeza Rais Dk.Samia kwa dhamira yake ya kufungua uwekezaji nchi kwa ili kuinua uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Wakili na Msuluhishi Stephen Msechu alisema sheria hiyo ni nzuri na imekuja kwa wakati muafaka na italeta tija kwa mashirika ya umma.
Ametaja vifungu ambavyo vitaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa mashirika kuwa ni pamoja na kifungu cha 15 ambacho kinatoa utaratibu shirikishi wa kuhamasisha mali za shirika la umma.
“Kifungu cha 16 kinahakikisha mashirika ya umma yanaongozwa na watu wenye uwezo. Kifungu kingine kinaeleza kuwa kiongozi mmoja haruhusiwi kuongoza taasisi zaidi ya moja hii inaongeza ufanisi na kugawa fursa kwa wengine,”amesema
Naye Mhariri Mkongwe Absolumu Kibanda amesema huo ni Muswada ambao msingi wake umejengwa kwa uzoefu wa mafanikio katika nchi zilizo na mfumo uliopendekezwa katika muswada wa uwekezaji unaowasilishwa.
“Kupitia mamlaka mpya Tanzania itakuwa na uwezo wa kuwaza kufikiria kuwekeza mitaji hadi nje ya nchi kwa namna ile wanavyofanya Singapore na China ambako taasisi za umma zinaweza kuwekeza mitaji nje ya mataifa yao,”amesema.
0 Comments