Header Ads Widget

SERIKALI ISICHONGANISHWE NA WANANCHI -MAKONDA.

 

Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP Tanga. 

WATUMISHI wa Serikali kutokuwajibika kwao kumekuwa chanzo cha wananchi kumchukia Rais na Serikali yake huku ikibainishwa kuwa  CCM hakitakuwa tayari kuwavumilia watumishi hao.


Kauli hiyo imetolewa na       Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa Paul Makonda wakati wa Mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Lamore Jijini hapa. 


Makonda alisema moja kati ya maelekezo kumi aliopewa na Rais Samia baada ya kupendekezwa na hatimae kuteuliwa ni kuwa sauti ya wananchi wa hali ya chini,wasio na pesa,vyeo wala elimu na kuwabaini wanao mchonganisha na wananchi wake.



Aidha alisema Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo na wajibu wa chama ni kuhoji miradi hiyo ili itekelezwe kwa wakati na iendane na thamani ya fedha zilizotengwa.


"Nina maelekezo kumi toka kwa Rais Samia,moja ni kuhakikisha je miradi inajengwa kwa wakati?kazi yangu na wenzangu kushughulika na wanaofanya ubadhilifu wa fedha hizo"Alisema Makonda.


Katibu huyo yupo Tanga kwa ziara ya siku mbili ikiwa na lengo la kukiimarisha chama kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wa 2024 na uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais 2025 ili kukidhi matakwa ya katiba ya Chama hicho ya kushinda chaguzi zote,kuunda dola na kuunda Serikali. 


Alisema mbali na hilo pia katika ziara hiyo ameitumia kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia majawabu yalikosekana kwa muda mrefu ambapo alitoa maelekezo mbalimbali kwa watumishi wa umma katika idara zilizolalamikiwa namna ya kumaliza kero za wananchi hao.


Makonda amekuwa na utaratibu wa kuwasimamisha mbele watumishi wa Serikali kutoka idara zote  kwenye Mikutano yake ya hadhara huku lengo lake likiwa ni kuwataka kutoa majibu kutokana na maswali ya wananchi lakini pia wananchi wajionea wenyewe wanao wasababisha waichukie Serikali yao kwa kushindwa kutoa huduma bora kwa wananchi. 


"Nafanya hivi ili wananchi mjionee wenyewe wanaoiangusha Serikali na  kuwafanya wananchi wamchukie Rais wetu na Serikali yake"Alisema Makonda. 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman alisema wanamshukuru Mh Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi Mkoani Tanga kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Komredi Rajabu alitumia fursa hiyo kumuomba Mh:Makonda kuweka mazingira rafiki kwenye  miradi yote inayotekelezwa Mkoani hapa ili iwanufaishe wazawa na kuwasaidia kuondokana na malalamiko ya wananchi kwa kushindwa kupata fursa ya ajira na kushindwa kunufaika na miradi  inayotekelezwa katika maeneo yao.


Nae Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba wakati alipopata nafasi ya kutoa salamu za mkoa alisema Mkoa uko salama na Serikali inamahusiano mazuri na Chama pamoja na Wazee jambo ambalo limeufanya Mkoa huu kuendelea kuwa shwari na kutokuwa na matukio ya Uvunjifu wa amani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI