Header Ads Widget

WAONYWA WASICHINJE WANYAMA KWAAJILI YA MATAMBIKO, WATUMIE KWA KITOWEO.

 

Matukio Daima, Moshi


WAUMINI wa Kanisa Katoliki wametakiwa kuachana na mila za kuchinja wanyama kwa ajili ya matambiko, badala yake nyama hizo zitumike kama chakula cha kawaida cha familia, kwani matambiko hayo hayana manufaa yoyote na mara nyingi huishia kuwa chakula cha mbwa.

Hayo yamesemwa na Paroko wa Parokia ya Maonano Mawela ambaye pia ni Vikari wa Vikariati ya Jimbo Katoliki Moshi, Padre Patrick Soka, wakati akizungumza baada ya ibada ya sikukuu ya Noeli yaani Christmas.

Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiweka nyama makaburini au maeneo ya nje kwa imani za kimila, jambo ambalo halina msingi wa kiimani wala kijamii, na badala yake linapoteza rasilimali ambazo zingetumika kuboresha maisha ya familia.



Pamoja na hilo, Padre Soka amewataka waumini kusimamia maadili kuanzia ngazi ya familia, kudhibiti matumizi ya simu hasa katika vikao na wakati wa kula ili kurudisha mazungumzo ya ana kwa ana, kujenga upendo, mshikamano na kusaidia kutatua changamoto za kifamilia.

Aidha, amelaani tabia ya vijana kushindanishwa katika unywaji wa pombe kali, akisema imekuwa chanzo cha vifo, kuharibika kwa afya, kupotea kwa nguvu kazi na kuporomoka kwa maendeleo ya familia, huku akisisitiza matumizi ya kiasi kwa wale wanaotumia.

Amesema baadhi ya wanaume wamegeuka kuwa chanzo cha migogoro kutokana na kulewa kupita kiasi na kurejea nyumbani usiku wa manane, jambo linalodhoofisha malezi na kuondoa amani majumbani.

Padre Soka ameihimiza jamii kuishi kwa upendo, kuhudhuria ibada, kuimarisha misingi ya kifamilia na kuiombea nchi amani kwa kuwa ikipotea madhara yake ni makubwa.


Pia amewakumbusha waumini wa Kanisa hilo kutoka ndani na nje ya Mawela Moshi kujitolea ujenzi unaoendelea kanisani hapo wa Groto chapel, ununuzi wa mavazi ya watumishi, kwaya ya watoto walioimba kwenye ibada ya misa ya kwanza kwa manufaa ya kukuza Imani na sehemu ya Ibada, Kwani Imani na sala huchangia amani ya familia na nchi kwa ujumla.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI