Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amefanya ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Shabaha - Jitegemee - New Land yenye urefu wa KM 8 iliyoko katika kata ya Mabogini.
Katika ziara yake hiyo, Prof. Ndakidemi aliongozana na Diwani wa Kata hiyo Dkt. Bibiana Massawe, Mainjinia kutoka TARURA na kampuni iliyopewa mkataba kuijenga barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 8 pamoja na viongozi wa vijiji, vitongoji na wananchi.
Akiwa katika ukaguzi huo, Prof. Ndakidemi aliishukuru TARURA na kampuni inayojenga barabara kwa kazi nzuri inayoendelea na kudai kuwa kwenye hizi barabara za changarawe, kinachotakiwa ni kuhakikisha inakuwepo mitaro ya kuchepusha maji kutoka barabarani.
Akikamilisha ziara yake katika kata ya Mabogini, Prof. Ndakidemi alitembelea na kukagua barabara ya Getifonga - Mabogini - Kahe ambayo imeharibiwa sana na mvua zinazoendelea mkoani Kilimanjaro.
Alijionea uharibifu mkubwa ambao umeifanya barabara hiyo isipitike na kuwafanya wananchi waandamane Januari 8 mwaka huu wakiiomba serikali iwasaidie ambapo Mbunge alifika na kuwapa wananchi pole ambapo aliahidi kwamba ataifikisha kero hiyo kwenye mamlaka husika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Diwani wa Kata ya Mabogini, viongozi wa vijiji na vitongoji na wananchi walimshukuru mbunge wao Prof. Ndakidemi kwa kuwasemea bungeni kwa lengo la kuwaletea maendeleo na kumwomba aibebe kero ya barabara ya lami kama hitaji lao kubwa.
Mwisho..
0 Comments