Na Thobias Mwanakatwe, MANYONI
MKUU wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Kemirembe Lwota ametoa msaada wa king'amuzi na vinywaji kwa wafungwa, mahabusu na watumishi waliopo katika gereza la Manyoni.
Ametoa msaada huo baada ya kutembelea gereza hilo akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Manyoni kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na gereza hilo.
Miradi aliyotembelea ni pamoja na kilimo cha mbogamboga na matunda, ufugaji pamoja na shughuli za ujenzi lakini pia huduma za kiafya.
Akizungumza na watumishi wa Jeshi la Magereza, Wafungwa na Mahabusu ameahidi kuhakikisha anakamilisha uwepo wa huduma ya upatikanaji wa maji katika gereza hilo ili shughuli za kilimo ziongezeke zaidi na miradi mingine inayotumia maji kuendelea.
" Kilimo kinachofanyika hapa kina tija sana, mnatupatia mbogamboga, matunda lishe bora kwa wananchi wetu, nimeanza kwa kuhakikisha kisima kimechimbwa sasa nitaendelea kusimamia Ukamilishaji wa hatua zinazofata ili uzalishaji uongezeke zaidi,"alisema Kemirembe.
0 Comments