Na Mbaruku Yusuph, Matukio Daima APP Tanga.
JESHI la Polisi Mkoani Tanga limefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa 107 kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya mauaji,wizi,unyang'anyi wa kutumia silaha na kupatikana kwa madawa ya kulevya na kuingia nchini bila ya kibali.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga Kamisha Msaidizi wa Polisi Almachius Mchunguzi alipozungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio ya Jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Oct 22 hadi Nov 27 mwaka huu.
Kamanda Mchunguzi alisema kati ya watuhimiwa hao,21 wamekamatwa na bangi kg 43,mirungi kg 124.5 na heroine gram 242, watuhumiwa 4 wamekamatwa kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu na watuhumiwa 7 ni Raia wa Ethiopia ambao wameingia Nchini bila ya kibali.
Alisema mtuhumiwa 1 amekamatwa kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha aina ya panga na watuhumiwa 74 wamekamatwa wakati Jeshi hilo likifanya doria zake za kuimarisha usalama wa raia na mali zao na upelelezi unaendelea ili waweze kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria zaidi.
Kamanda Mchunguzi alisema katika hatua ya kuimarisha doria za nchi kavu na bahari Nov 21 katika maeneo ya kisiwa cha Jembe Wilaya ya Tanga Mjini Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata boti aina ya Febre isiyokuwa na usajili iliyokuwa na injini aina ya Yamaha HP 15 na vifaa mbalimbali vya kuvulia samaki.
Alisema katika doria hiyo watuhumiwa walikimbia na kulitelekeza boti hilo sambamba na chupa za hewa za oxygen 2,mipira ya kupumulia 2,Tanga la kuokotea samaki,kiberiti,na kg 30 za samaki wa aina mbalimbali walivuliwa kwa kutumia baruti ambao wamethibitishwa na Afisa uvuvi kuwa samaki hao hawafai kwa matumizi ya binaadamu.
Kamanda Mchunguzi alisema mbali ya matukio hayo Jeshi hilo limefanikiwa kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa 41,kesi 11 zinaendelea mahakamani na kesi 27 zimetolewa hukumu mbalimbali ambapo watuhumiwa 3 Justis Kunael (40),Said Adam(32) na Maliki Amiri (38)wakazi wa Wilaya ya Handeni walihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kubaka.
Aidha Kamanda huyo alisema kulitokea tukio la mauaji ambapo watuhumiwa Rashidi Mwalimu,Siwajui Kigaa,na Zuberi Hassan wote wakazi wa Kijiji cha Kwadugwa Wilayani Handeni ambao walihukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa.
Vilevile Kamanda huyo alisema Nov 18 Jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata Hamis Kombo mkazi wa kwediboma (46)Wilayani Kilindi akiwa na wenzake nane ambao ni waganga wa kienyeji ambao wanajihusisha na ramli chonganishi.
Watuhumiwa hao wakiwa katika Kijiji cha kivindai,kata ya Tongoni,Tarafa ya Pongwe Wilaya ya Tanga Mjini ambapo wananchi wa kijiji hicho waliwaita waganga hao kwa ajili ya kufanya uchunguzi katika nyumba za Kijiji hicho ambazo zinasadikiwa kuwa na uchawi .
Alisema wanakijiji hao wamekuwa wakilalamika kufanyiwa vitendo vya kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo na kuachwa wakiwa watupu kimazingara wakati wakiwa wamelala usiku na watuhumiwa hao wapo nje kwa dhamana.
Hata hivyo Kamanda Mchunguzi alitumia fursa hiyo kuwashukuru raia wema kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kutoa taarifa ambazo zimefanikisha Jeshi hilo kukamata wahalifu na mali zilizoibiwa.
0 Comments