NA ARODIA PETER, MATUKIODAIMA App DAR
Waziri wa Nishati, Dr Dotto Biteko ameshauliwa kuunda Tume ya kuchunguza ubadhirifu katika miradi ya umeme iliyoingiwa na mtangulizi wake, Januari Makamba.
Dr. Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu amepewa ushauri huo na kijana anayejiita Mzalendo, David Mkindikwa leo Novemba 28, 2023 mjini Dar es Salaam.
Mkindikwa ametoa ushauri huo wakati akifanya uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/2023 kwa waandishi wa habari.
Amesema endapo Dr. Biteko hatochukua hatua za haraka kubaini na kuweka wazi hujuma zilizopo kwenye sekta ya nishati basi na yeye ataingia kwenye mtego wa uchafu wa watangulizi wake.
Akitoalea mifano, Mkindikwa amesema kuanzia mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya kifo cha hayati John Magufuli na kuondolewa kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani taifa lilianza kutumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa mgao wa umeme.
"Ikumbukwe kuwa mgao wa umeme nchini ulikuwa umekoma kwa zaidi ya miaka sita mfululizo, vile vile, kupanda kiholela kwa bei ya nishati ya mafuta viliibuka baada ya Januari Makamba kuteuliwa kwenye wizara hiyo.
"Uchambuzi wa Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 imeonyesha ufisadi mkubwa kwenye Wizara ya Nishati lakini kwa bahati mbaya hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na kwa bahati mbaya kama nchi tunajielekeza kujadili mambo madogo madogo huku nchi yetu ikiteketea.
Mkindikwa ambaye amejipambanua kuwa anazungumza hadharani kwa kusukumwa na uzalendo wake, amesema kushindwa kwa wizara ya nishati kusimamia kikamilifu mkataba wa mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JHNPP-2115) kutokana na faini ya ucheleweshaji na CSR na kumeisababishia nchi hasara ya Sh bil 598 katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Ameongeza kuwa, serikali kutokudai tozo ya fidia ya ucheleweshaji wa mkataba ambayo ni asilimia 5 ya mkataba, kiasi cha Sh bil 328 zimepotea.
"Kampuni ya Arab Contractor haijadaiwa fidia ya ucheleweshaji ya mwaka mzima kama mkataba unavyosema, licha ya kuendelea kuilipa kampuni hiyo kila inapowasilisha hati ya madai.
"Tumemsikia mara kwa mara aliyekuwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Januari Makamba akipiga porojo badala ya kujibu hoja za wabunge na CAG, hii ni dhahiri kwamba yeye na Menejimenti ya TANESCO wamekula njama ya kuiibia nchi kiasi cha shilingi Bilioni 328.
"Pia ikumbukwe kuwa hata katika mwaka wa fedha 2022/2023 Kampuni ya Arab Contractor inapaswa kuwa imetozwa faini kiasi cha shilingi Bilioni 328 na hivyo kufanya madai yote ya fidia ya ucheleweshaji kufikia shilingi bilioni 656." amesema Mkindikwa na kuongeza kuwa:
"Serikali imeshinda kesi mahakamani dhidi ya IPTL tangu Machi 2021 na kutakiwa kulipa Sh bil 370, lakini TANESCO imeshindwa kuzidai fedha hizo. Lakini jambo la kusikitisha kila suala hili lilipohojiwa bungeni halikuwa kupata majibu ya maana.
"Huu ni ufisadi uliopitiliza na unalenga kumchonganisha Mheshimiwa Rais na wananchi wake ili aonekane hana uchungu na nchi.
"Mheshimiwa Dotto Biteko haya mambo umeyakuta yakifanywa na mtangulizi wako, hivyo kwa maslahi ya Taifa fanya uchunguzi wa haraka ili kujinusuru." amesema
0 Comments