Na Fadhili Abdallah,Kigoma
HALMASHAURI ya wilaya Kibondo mkoani Kigoma imesema kuwa ukarabati na maboresho makubwa yaliyofanywa kwenye soko kuu la Halmashauri hiyo lililopo mjini Kibondo utaongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kwa kiasi kikubwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kibondo, Stephen Junks akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo alisema kuwa awali halmashauri ilikuwa ikikusanya kiasi cha shilingi milioni 15 kutokana na hali ya soko iliyokuwa wakati huo ambapo ilikuwa ni vibanda vya mbao na meza za magunia.
Kutokana na ukarabati na uboreshaji huo Junks alisema kuwa halmashauri imekadiria kukusanya kiasi cha shilingi milioni 250 kwa mwezi kwa ukodishaji vibanda vya maduka lakini pia vizimba ambavyo vimeboreshwa tofauti na hapo awali ambapo halmasgauri ilikuwa ikikusanya ushuru wa shilingi 500 mara mbili kwa wiki kwa kila mfanyabiashara.
Akitoa taarifa kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo Kaimu Mkuu wa idara ya miundo mbinu ya halmashauri ya wilaya Kibondo, Edwin Edward alisema kuwa kiasi cha shilingi 576 milioni kinatarajia kutumika kukamilisha mradi huo ikiwa ni fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Eward alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo wanatarajia kujenga maduka 66 ambapo maduka 26 yapo kwenye hatua ya ukamilishaji na maduka 20 yapo kwenye hatua ya msingi na tayari idadi kubwa ya wafanyabiashara wamefanya maombi kuomba vibanda vya kufanya biashara.
Baadhi ya wananchi wa mjini Kibondo waliokuwa wanafanya biashara katika eneo hilo akiwemo Salma Omari ambaye alisema kuwa awali soko hilo lilikuwa ni la vibanda na vichanja vilivyokuwa vinafunikwa na magunia na turubai hivyo wakati wa mvua au jua kali hali ilikuwa ngumu sana na kwa sasa wamejengewa vizimba na kuweka bati wanaamini watafanya biashara vizuri.
Mwisho.










0 Comments