NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Waziri mkuu mstaafu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe;Mizengo Pinda amesema kuwa miaka 50 ya taasisi ya utafiti na maendeleo ya mbogamboga Duniani kanda ya Mashariki na kusini mwa Afrika imewezesha upatikanaji wa lishe kwa watu kupitia uzalishaji wa mbogamboga ma matumizi ya teknolojia hivyo ni muhimu watunga sera kuona umuhimu wa kukikuza kilimo hicho ili kukidhi mahitaji ya chakula mijini.
Waziri Pinda aliyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo yaliyofanyika mkoani Arusha ambapo alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika kilimo hicho ikiwemo kujenga vyumba vya baridi kwaajili ya kutunza mazao katika masoko ili kuweza kupunguza uharibifu wa mazao yanayopelekwa katika masoko kwani zisipotunzwa vizuri huaribika kwa haraka na kutupwa.
“Kumekuwa na ongezeko kubwa la watu katika miji yetu ya Afrika katika suala zima la lishe, lakini pia kumekuwa na tatizo la watu kuongezeka uzito uliopitiliza kutokana na mitindo ya maisha na vyakula wanavyokula hivyo ni wakati muafaka sasa wa kuhamasisha kilimo na ulaji mbogamboga kwa afya bora ya watu wetu,” Alisema waziri mkuu Mstaafu.
Alifafanua kuwa tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo zimesaidia kulinda mbogamboga dhidi ya wadudu na mlipuko wa magonjwa ya mimea, kupunguza upotevu wa mazao ya mbogamboga ikiwa ni pamoja na utimilifu wa sekta ya kilimo cha bustani na kuongeza chakula na usalama wa lishe kwa mamilioni ya wakulima wadogo na watumiaji wa mbogamboga.
kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara ya kilimo ,umwagiliaji, mifugo na maliasili Zanzibar Seif Mwinyi alisema kuwa miaka 50 ya taasisi hiyo ni kipindi pekee kinachoonyesha uvumilivu, ubunifu, dhamira yao ya kutoa suluhisho la changamoto ya masuala ya kilimo na lishe Duniani.
“Miaka 50 inawakailisha miaka ya ujuzi, maarifa na uzoefu ambao World vegetable imejenga katika kipindi chote cha huduma zake hapa Tanzania na Duniani kwa ujumla katika kujenga dunia endelevu yenye chakula bora na lishe kwa kila mtu,” Alisema.
Naye Mkuu wa wilaya ya Arumeru Emanuela Kaganda akiongea kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela alisema kuwa tasisi hiyo imeonyesha umuhimu mkubwa wa kuwepo katika mkoa wa Arusha kwani imewajengea uwezo wakulima wadogo zaidi ya 1000, imewezesha shule zaidi ya 50 za sekondari na msingi na kuweza kuwanufaisha wanafunzi zaidi ya 5000 kupitia mradi wa bustani mashuleni na kwenye kaya.
“Wakulima na wanafunzi wameweza kujifunza vizuri namna ya kushiriki kilimo cha mbogamboga na kuweza kuboresha lishe wanavyokula mashuleni na katika kaya ikiwemo kuokoa fedha ambazo zingetumika kwaaajili ya kununua mbogamboga,” alieleza.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt Gabriel Rugelema aleleza kuwa wanajivunia kazi waliyoifanya kupitia sayansi katika kuendeleza mazao ya mboga na wataendelea kufanya kazi hiyo kwa manufaa ya Dunia nzima ambapo kama taasisi ya umma ya utafiti wana wajibu wa kipekee katika kuleta mafanikio katika mazao ya mboga.
“Kama tukipotea hivi sasa tutakumbukwa na Dunia kwani sisi ndio taasisi ya kipekee Duniani wenye wajibu wa kufanya utafiti, uendelezaji na uhamasishaji wa mazao ya mboga mboga na matunda kwa hiyo tungepotea leo kwa sababu yoyote ile Dunia itakuwa masikini kwa sababu hatupo,” Alieleza Dkt Rugelema.
Alifafanua kuwa kupitia benki yao ya mbegu tuna zaidi ya aina tofauti tofauti za mbegu 7500 na zaidi ya 6800 nchini Taiwan ambapo pia wako katika ujenzi benki ya vinasaba vya mbegu kwa ufadhili wa serikali ya Swatini na wanafanya kazi na mtandao SADIC ambapo baada ya kukamilika watakuwa ni sehemu pekee ya benki ya mbegu za mbogamboga Afrika kwasasa na kizazi cha baadae.
0 Comments