Na Matukio Daima Media , Mufindi
Mgombea ubunge jimbo la Mufindi Kusini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chavala Yohannes Matonya, amesema kero kubwa inayowakabili wananchi wa jimbo hilo ni upatikanaji wa maji safi na salama, kutokana na miundombinu duni na miradi mingi ya maji kutotekelezwa kikamilifu. Akiwa katika ziara zake za kampeni katika kata mbalimbali, Matonya amesema ni wakati wa wananchi wa Mufindi Kusini kuchagua kiongozi atakayewawakilisha kwa vitendo, si kwa maneno.
Alisema licha ya serikali kufanya juhudi kubwa katika miaka ya hivi karibuni, bado maeneo mengi ya jimbo hilo yanakumbwa na tatizo la ukosefu wa maji, hasa katika kata za Luhunga, Mninga, Igowole, Nyololo, Malangali, Ihowanza, Idunda, Mtambula na Itandula ambapo wananchi hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali inayochangia kurudisha nyuma shughuli za maendeleo na kuathiri afya hasa kwa kina mama na watoto.
“Miundombinu ya maji bado ni kero kubwa kwa wananchi wa Mufindi Kusini. Watu wetu wanaamka alfajiri kwenda kutafuta maji, watoto wanakosa muda wa kujisomea, wagonjwa hawapati huduma bora katika vituo vya afya kutokana na ukosefu wa maji,Mimi Chavala Matonya naomba nitumwe kuwa mbunge wa jimbo hili, ili kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali, tuwekeze nguvu kubwa katika kutatua kero hii,” alisema Matonya.
Matonya ameeleza kuwa anayo dhamira ya dhati kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, huku akiahidi kusimamia kikamilifu upatikanaji wa fedha kutoka serikalini na kwa wahisani ili kuhakikisha kila kata inakuwa na huduma ya maji inayotegemewa.
Changamoto ya Afya
Mbali na tatizo la maji, Matonya alitaja changamoto nyingine zinazolikabili jimbo hilo kuwa ni pamoja na hali ya miundombinu ya vituo vya afya, upatikanaji wa dawa na uhaba wa watumishi wa afya waliobobea.
Alisema kuwa baadhi ya vituo vya afya vilivyoboreshwa bado vinakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba, ukosefu wa dawa muhimu, na watumishi wa kutosha hali inayohatarisha maisha ya wananchi.
“Kituo cha afya siyo tu jengo, bali ni huduma. Kama hakuna dawa, hakuna wauguzi wa kutosha, hakuna huduma za dharura, basi tuna matatizo makubwa. Nitahakikisha tunasimamia ajira mpya, usambazaji wa dawa na uboreshaji wa vifaa tiba ili wananchi wetu wapate huduma bora,” alisisitiza.
Elimu na Wasichana
Matonya alisema katika sekta ya elimu, Matonya amesema ukosefu wa miundombinu ya hosteli kwa wasichana katika shule nyingi za kata ni changamoto inayowarudisha nyuma wanafunzi wa kike, hususan katika kipindi cha mabadiliko ya mwili au wanapolazimika kusafiri umbali mrefu kwenda shuleni.
“Tutahakikisha tunajenga hosteli za kisasa kwa wasichana katika shule mbalimbali ili kuwawezesha kusoma katika mazingira salama, yasiokuwa na usumbufu. Hii itasaidia kupunguza utoro, kuongeza ufaulu na kuwaandaa wasichana wetu kushika nafasi za uongozi wa kesho,” alisema Matonya
Uhifadhi na Uchumi wa Kijani
Akizungumzia masuala ya mazingira, Matonya ameahidi kuanzisha ushirika wa kupanda miti ya biashara kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kusaidia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza uchumi wa kijani katika jimbo hilo. Ametaja kuwa miradi kama hiyo huwezeshwa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, hivyo kuna fursa kubwa ya kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu.
“Kupitia ushirika huu wa miti ya biashara, tutapunguza uharibifu wa mazingira, tutasaidia vijana kupata ajira, na kuongeza mapato ya familia. Hii ni njia ya kisasa ya kuunganisha mazingira na uchumi,” alisema.
Kutoa Fursa kwa Vijana Wanaofaulu
kuwa katika kuongeza fursa kwa vijana, Matonya ametangaza mpango wake wa kugharamia watoto 16 kila mwaka watakaofaulu vizuri katika masomo yao kwenda kusoma nje ya nchi katika fani mbalimbali. Amesema mpango huu utalenga vijana kutoka familia duni lakini wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma.
“Nia yangu ni kutoa fursa kwa watoto wetu wenye vipaji lakini hawana uwezo wa kifedha kuendeleza masomo yao. Nitashirikiana na mashirika ya ndani na nje kuhakikisha kila mwaka vijana 16 wa Mufindi Kusini wanakwenda kusoma nje ya nchi, wawe madaktari, wahandisi, walimu, wataalamu wa TEHAMA na wengineo. Tutaleta mabadiliko ya kweli,” alisema kwa msisitizo.
ChavalaYohannes Matonya amewataka wananchi wa Mufindi Kusini kumchagua kuwa mbunge wao, akiahidi kuwa hatakuwa mbunge wa maneno bali wa vitendo.
Amesema ana uchungu wa kweli kwa maendeleo ya Mufindi Kusini, na kwa kushirikiana na viongozi wengine wa chama na serikali, anaamini kero nyingi zinazowakabili wananchi zitapatiwa ufumbuzi.
“Mimi ni kijana wa Mufindi, ninayajua matatizo yetu kwa undani. Sitahitaji kuambiwa na mtu, ninao uzoefu, dhamira na uwezo wa kushirikiana na taasisi mbalimbali kubadilisha maisha ya wananchi. Tuunganishe nguvu, Mufindi iwe ya mfano,” alisema Matonya
1 Comments
Ni wakati sasa kwa Wanamufindi Kusini Kuamua kumtuma Kijana wetu mwenye nia dhabiti na tusiye na shaka nae.. Viva Comrade👏👏
ReplyDelete