Mtwara, Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya Tandahimba limeadhimia kila kijiji kutengeneza madawati 15 hatua ambayo itapunguza uhaba uliopo kwa sasa.
Akizungumza jana katika Kikao cha Baraza la Madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Baisa Abdallah Baisa alisema kila kijiji kinapaswa kuona jambo hilo kwa uzito wake.
kampeni hiyo inalenga kumuondoa mtoto chini na kumuweka katika dawati na kuboresha mazingira ya kusomea na kujifunzia ambapo rasimali zilizopo ndani ya wilaya zitatumika ili kuepuka gharama kubwa za utengenezaji wa madawati hayo.
“Elimu ndio msingi wa maisha kitendo cha watoto wengine kukaa chini na wengine kukaa kwenye madawati kunadhoofisha watoto hao na kujiona hawana usawa haiwezekani wengine wakae chini na wengine kwenye dawati”
Nae Diwani Kata ya Nanyhanga Abbas Shaibu Namanela alisema kuwa kampeni hiyo ni nzuri na ina malengo mazuri yakuweza kuboresha na kunyanyua elimu katika wilaya hiyo.
“Unajua tunao wanafunzi wengi shule za msingi ili kuweza kuwaboreshea mazingira ndani ya darasa hatuna budi kuungana na kufanya hii kampeni ili iweze kufanikiwa ni wazi kuwa mahitaji yapo tumelipokea na tunaenda kuhamasisha zaidi kwenye vijiji vyetu” amesema Namanela
kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Kanal Patrick Sawala alisema kuwa tunaoupungufu wa madawati 3000 na mahitaji ya miundombinu mingine ikiwemo madarasa, vyoo pamoja na nyumba za walimu.
“Tumeweka mikakati Wilaya ya kuhakikisha kuwa miundombinu inaboreshwa ifikapo mwaka 2024 yaani asiwepo mtoto anakaa chini kwenye sakafu ili tunapopita kuboresha elimu ndani ya Wilaya ya Tandahimba” amesema Sawala
0 Comments