Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
BARAZA la madiwani Halmashauri ya wilaya ya Njombe mkoani Njombe limewaonya baadhi ya maofisa watendaji na watumishi walevi wakati wa kazi na kusababisha uwajibikaji duni unaoiletea hasara serikali.
Onyo hilo limetolewa na mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Valentino Hongoli wakati wa kikao cha baraza la madiwani la Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 ambapo amesema vitendo hivyo vimekuwa kikwazo katika kumsaidia Rais kutekeleza majukumu katika maeneo yao jambo ambalo halitofumbiwa macho.
Sanjari na hilo lakini pia Hongoli amewataka maofisa watendaji kwenda kutekeleza maagizo ya baraza la kuhesabu ubao kwa ubao kwenye magari ya mbao ili kudhibiti utoroshwaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri.
Nao baadhi ya madiwani akiwemo Roida Wandelage,Innocent Gwivaha na Javan Ngumbuke wamesema hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa kwa maofisa watendaji wazembe na walevi.
Hata hivyo kituo hiki kimezungumza na baadhi ya maofisa watendaji Kata akiwemo John Mhina na Hilda Nyudike ambao wamekiri kuwapo kwa changamoto hizo kwa baadhi yao na kwamba wataendelea kuzifanyia kazi.
0 Comments