Na Matukio Daima Media
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewaonya vikali makatibu na watendaji wake wa ngazi mbalimbali dhidi ya kuwatoza wanachama fedha zaidi ya viwango rasmi vilivyowekwa wakati wa kuchukua fomu za kuwania nafasi za ubunge na udiwani.
Onyo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa baadhi ya watendaji wa chama hicho.
Makalla amesema kuwa chama kimepokea taarifa kutoka maeneo mbalimbali zinazoonyesha kuwa baadhi ya watendaji wamekuwa wakiwatoza wanachama fedha zaidi ya kiwango kilichowekwa kisheria na chama, ambacho ni shilingi 500,000 kwa waombaji wa ubunge na shilingi 50,000 kwa waombaji wa udiwani.
Amesisitiza kuwa hakuna ada ya ziada inayoidhinishwa na chama zaidi ya hizo, na kuwa vitendo vya kutoza fedha nje ya utaratibu ni ukiukwaji wa maadili ya chama na vinaweza kuchukuliwa kama viashiria vya rushwa.
Makalla amesema CCM haitasita kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo, kwa kuwa vinaathiri uaminifu wa mchakato wa ndani ya chama na kudhalilisha misingi ya haki na usawa kwa wanachama wote.
Aidha, amewataka wanachama wote wanaokusudia kugombea nafasi hizo kutoa taarifa kwa uongozi wa juu wa chama pindi watakapodaiwa fedha zaidi ya kiwango rasmi, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watendaji hao.
Amewasihi watendaji wote wa chama kufuata maadili, kuzingatia taratibu na kuepuka tamaa ya kujinufaisha binafsi kwa mgongo wa chama, hasa kipindi hiki muhimu cha maandalizi ya uchaguzi.
CCM inaendelea na maandalizi ya mchakato wa kupokea na kuchuja wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea uchaguzi mkuu ujao, ambapo uwazi, uadilifu na uzingatiaji wa kanuni umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha mchakato huo unakuwa huru na wa haki.
0 Comments