(Matukio Daima)
Asasi za Kiraia zaidi ya 15 nchini ambazo yanajihusisha na utetezi wa haki binadamu, ikiwemo Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania (THRDC), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) wamelaani vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyodaiwa kuendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini yanayozunguka hifadhi za wanyama pamoja na maeneo mengine mbalimbali ya maliasili.
Akisoma tamko la pamoja, Mkuu wa Dawati la Utetezi THRDC, Wakili Paul Kisabo amesema katika maeneo mbalimbali nchini mifugo imekuwa ikikamatwa kinyume na utaratibu huku akitolea mfano eneo la Ngorongoro, ambapo amedai kuwa wafugaji mifugo yao imekuwa ikikamatwa na maafisa wanyamapori kisha kuwataka watoe kiasi kubwa cha pesa.
"Tunalaani vikali ukiukwaji wa haki za mifugo katika wilaya ya Ngorongoro na maeneo mengine kote nchini ambapo mifugo imekuwa ikikamatwa kinyume cha Sheria, kuuzwa ama kutaifishwa Kinyume cha Sheria na Katiba ya nchi yetu."
Amesema kuwa kwa upande wa Ngorongoro licha ya kuwepo zuio la Mahakama kuhusu Utekelezaji wa Tangazo lililotolewa na Rais Na. 604 la Mwaka 2022 usimame kuanzia tarehe 22.08.2023 hadi kesi ya msingi itakapoisha kwa kutolewa uamuzi na Mahakama, wamedai kumekuwepo na ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na mifugo kukamatwa na watu kutozwa faini ya laki moja kila mmoja.
"Tunalaani vikali vitendo vyote ambavyo vimeonekana kupuuza ama kudharau maamuzi na amri halali za Mahakama ana kupelekea mifugo kuuzwa kinyume cha Sheria za nchi yetu."
Amesema "Mnamo tarehe 19.09.2022, Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha ilitoa uamuzi juu ya Tangazo la Waziri wa Mali Asili na Utalii Na. 421 la Mwaka 2022 ambapo
pamoja na mambo mengine Mahakama ilitamka kuwa Tangazo la Waziri halikufuata utaratibu wa Kisheria hasa kuwashirikisha wananchi wakazi wa vijiji hivyo, Kata, Halmashauri ya Wilaya pamoja na wahanga wa Tangazo hilo.
Ameongeza kuwa "Katika uamuzi huo, Mahakama ilisisitiza kwamba:
(a) Pori Tengefu la Pololeti lenye kilometa za mraba 1,502 halikutangazwa kwa
kufuata Sheria na lilikufa mara baada ya Rais kutangaza kuwa eneo hilo ni Pori la Akiba kupitia Tangazo la Serikali Na. 604 la mwaka 2022 na hivyo kwa sasa hakuna kitu chochote kiitwacho Pori Tengefu la Pololeti
(b) Utekelezaji wa Tangazo lililotolewa na Rais Na. 604 la Mwaka 2022 usimame
kuanzia tarehe 22.08.2023 hadi kesi ya msingi itakapoisha kwa kutolewa uamuzi
na Mahakama."tamko hilo limeeleza
Wametoa wito kwa Serikali wakitaka hatua zichukuliwe "Tunatoa wito kwa Serikali kuwachukulia hatua za kisheria watumishi na viongozi wa Serikali walioshiriki katika ukiukwaji wa amri za Mahakama. Lengo ni kuhakikisha kwamba watumishi hao wanaheshimu na kulinda utawala wa Sheria na katiba ambayo waliapa kuilinda."
Aidha wamesema kuwa hali hiyo ya ukiukwaji wa haki za binadamu inatokea kwenye maeneo ya Loliondo, Mbarali, Msoma, Tarime na kwenye maeneo mengine, ambapo katika tamko hilo wamedai kuwa kuna baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa na wasiwasi na baadhi ya watumishi wa Mahakama ambao utoa uamuzi mbalimbali kwenye masuala yenye migogoro inayowahusu wafugaji.
Hata hivyo wametoa wito kwa mahakama ya Tanzania kufuatilia utekelezwaji wa uamuzi wake.
"Tunatoa wito pia kwa Mahakama ya Tanzania kufuatilia utekelezaji wa maamuzi yake kwa wivu mkubwa, sisi tunaamini kwamba maamuzi ya Mahakama ni maamuzi ya haki na hivyo yanapaswa kutekelezwa na kila mtu kama yalivyoamuliwa." tamko limeeleza
Aidha wametoa wito kwa Mwanasheria kutekeleza uamuzi wa Mahakama kwenye masuala mbalimbali ambayo tayari yameamriwa .
"Tunatoa wito wa jumla kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutekeleza maamuzi
mbalimbali ya Mahakama kisheria. Mfano maamuzi ya Mahakama za ndani, za Kikanda na Kimataifa. Maamuzi hayo ni kama ya kesi ya Rebecca Gyumi, Maria Mushi, Mjomba Mjomba, Kesi ya THRDC, LHRC na MCT iliyoamuliwa na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mwaka 2019, THRDC na LHRC iliyoamuliwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, kesi za Mch. Mtikila, kesi ya Jebra Kambole na kesi ya Bob Wangwe ya Wakurugenzi wa Uchaguzi "limeeleza tamko hilo.
Hata hivyo itakumbukuwa kufuatia kuwepo kwa baadhi ya malalamiko kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye baadhi ya maeneo yaliyotajwa baadhi ya viongozi kutoka kwenye mamlaka za Kiserikali zinazosimamia maeneo hayo kuna wakati wamekuwa wakidai kuwa baadhi ya wafugaji wamekuwa wakikahidi na kuingiza mifugo kwenye maeneo yasiyo rasimi kisheria.
Mashirika mengine ambayo yameungana kutoa tamko hilo ni Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), Shirika la Uraia na Msaada wa Kisheria (CILAO) , Mtandao wa Mashirika ya Kifugaji (PINGOs Forum) , Ujamaa Community Resource Team (UCRT) , Shirika la Kukuza Haki za Binadamu (OPH)
, Shirika la Uhifadhi wa Mifumo ya Asili na Jadi (TEST), Shirika la Maendeleo Jumuishi Wilayani Ngorongoro (IDINGO),Jukwaa la Ardhi Tanzania, Shirika la Kuinua na Kusaidia Maisha ya Wafugaji (PALISEP), Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), Green Planet Initiative (GPI), Pan African Lawyers Union (PALU).
0 Comments