Header Ads Widget

WADAU WATAKIWA KUHAKIKI USAHIHI WA VIPIMO VYA VIFAA VYAO

Na Adery Masta 

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wadau mbalimbali kuchangamkia huduma ya uthibitishaji wa mifumo (System Certification) inayotolewa na shirika hilo kwa gharama kidhi kabisa.

Aidha, shirika hilo limewataka wadau hao kufika kwenye banda la TBS lililopo kwenye Maonesho ya 49 Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa au ofisi za shirika zilizopo karibu nao ili kupata maelezo kuhusiana na namna wanavyoweza kupata huduma hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Meneja Uhusiano na Masoko wa TBS, Gladness Kaseka, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo maarufu kama ya Sabasaba.

Kaseka alitoa wito kwa wizara, ofisi za serikali , taasisi za umma na nyingine za sekta binafsi kuwa na imani kabisa kwamba TBS wanaweza kutoa huduma hiyo ambayo walikuwa wanaipata kutoka kwenye kampuni za nje.


" Huduma hiyo inapatikana TBS na tuna Ithibati ya kutoa huduma hiyo hapa nchini," alisisitiza Kaseka.


Kwa upande wa wale wanaotoa huduma mahospitalini, wenye miradi ya ujenzi na wenye viwanda, Kaseka alisema TBS ina huduma ya metrology (ugezi) kwa ajili ya uhakiki usahihi wa vipimo wa vifaa vyao.


Alifafanua kuwa wamekuwa wakisikia wateja wanalalamika kwamba wamepimwa wamekutwa wana shida, lakini wanapoenda kwingine wanaambiwa hawana shida.


"Hiyo inawafanya watoa huduma wapoteze imani kwa wateja, kwa hiyo TBS tupo kwa ajili ya kuhakiki vipimo wanavyotumia hospitalini.


Tunakaribisha wenye hospitali, wenye miradi ya ujenzi na wenye viwanda kufika kwenye shirika letu kupata huduma ya ugezi," alisema.


Alisema TBS inahakiki vipimo vinavyotumika katika maabara, ambapo uhakiki huo unawasaidia kuweza kutoa majibu sahihi ya mgonjwa kama ni hospitalini na kama ni viwandani inawasaidia kujua kwamba wanatumia malighafi sahihi katika kutengeneza bidhaa ambazo wanazalisha.


Alifafanua kwamba huduma hiyo inatolewa TBS kwa kuwafuata wahusika katika maeneo yao ya kazi iwe hospitali au viwandani kwa ajili ya kuhakiki vipimo vyao.


Alisema huduma hiyo wanaitoa kwa upana wake na kwa umahiri . Kuhusu mrejesho wa watu kujitokeza kupata huduma hiyo, alisema ni mkubwa, lakini wanapenda hospitali zote zipate huduma hiyo kwa sababu ni eneo muhimu sana zikiwemo zile zinazojiona ndogo (zahanati) kwani wanapohudumia mtu anapenda kuwa na majibu ya uhakika.


Alisema TBS haipendi kuona hospitali zinapoteza wateja kwa kutokutoa majibu ya uhakika kwani ni watu ambao wamefanya uwekezaji mkubwa na kuna watu ambao wameajiriwa pia.


Aliongeza kwamba tayari wameishaanza kutembelea hospitali kwa ajili ya kufanya ugenzi na kutaka wale ambao hawajafikiwa waanze kwenda wenyewe TBS kupata huduma hiyo.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI