NA CHAUSIKU SAID,MATUKIO DAIMAAPP MWANZA
Maisala Ramadhani (25) Mkazi wa kisiwa Cha Maisome Wilaya Sengerema Mkoani Mwanza ameangua kilio mahakamani baada ya kuhukumiwa jela miaka 20 baada kukiri kosa la kukutwa na dawa za kulenya aina ya Bangi nyumbani kwake.
Hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba 121/2023, imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka.
Awali, akisoma maelezo mbele ya hakimu, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Morice Mtoi alisema mshitakiwa alikamatwa Oktoba 9, 2023, na Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa Wilaya ya Sengerema, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Titho Mohe.
Mwendesha mashtaka huyo alisema mshtakiwa alikamatwa na askari huyo katika kisiwa cha Maisome kambi ya wavuvi ya Migongo akiwa na Bhangi kilogramu 10 kwenye nyumba yake ya kuishi.
Wakili wa Serikali, Morice Mtoi alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na Kifungu namba15A(1) (2)(c) Cha sheria ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya Sura ya 95 toleo la mwaka 2019 kama ilivyofanyiwa mabadiliko na sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali namba 5 ya mwaka 2021.
Pamoja na maombi ya mshtakiwa (Maisala) kuomba kupunguziwa adhabu, Mahakama imemhukumu kifungo hicho cha miaka 20 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo kulingana na madhara yasababishwayo na madawa ya kulevya.
0 Comments