Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP.
KAMPUNI ya China ya CRJE inayotekeleza mradi wa ujenzi wa majengo ya Wizara ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia imetakiwa kuongeza nguvu kazi na muda wa kazi ili kuhakikisha jengo hilo linakabidhiwa ifikapo Disemba 15, 2023 kulingana na makubaliano ya mkataba.
Kauli hiyo imetolewa Nov Mosi,2023 na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo jipya la Ofisi za Wizara hiyo lililopo katika Mji wa kiserikali Mtumba ili kujionea maendeleo ya mradi huo.
"Jengo limefikia asilimia 80, kwa hatua hii Mkandarasi amejitajidi, na amenihakikishia kwamba watakabidhi jengo kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba" alisema Prof. Nombo
Aidha Katibu Mkuu huyo ameishukuru kampuni ya ABBEC kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi ambayo ndio Mshauri Elekezi wa mradi wa ujenzi huo kwa kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Mkandarasi na kwamba hali hiyo itasaidia kutekeleza mradi kwa ufanisi na kwa wakati.
Ameongoza kuwa wakati kazi zingine za nje ya jengo zikiendelea, Wizara itawasiliana na Mamlaka nyingine ili kuhakikisha miundombinu mbalimbali katika jengo hilo nayo inakamilika kwa wakati.
Akizungumza kufuatia ziara hiyo, Meneja wa mradi wa Kampuni ya China ya CRJE Li Yang ameishukuru serikali kuwapatia nafasi ya kutekeleza mradi huo, ambapo ameahidi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na kukabidhi kwa wakati.
Kwa upande wake Mhandisi Renatus Dominic kutoka Kampuni ya ABBEC ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambayo ndio Mshauri Elekezi wa mradi huo, amemhakikishia Katibu Mkuu Wizara ya Elimu kwamba watashirikiana kikamilifu na Mkandarasi waweze kukabidhi jengo hilo kwa muda uliopangwa.
"Tunakushukuru Katibu Mkuu kwa kututembelea ili ujionee kinachoendelea na labda tukuahidi sisi tutaendeleza ushirikiano na Mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi wa mradi huu kwa wakati kama ulivyopangwa" alisema Mhandisi Dominic
Akifafanua zaidi kuwa kazi zinazoendelea ndani ya jengo hilo ,Mhandisi Dominic alisema ni pamoja na kupaka rangi na kuweka miundombinu ya huduma wezeshi za jengo.
0 Comments