Header Ads Widget

WINGI WA WANAFUNZI NA MAPATO SIO VIPIMO KWA VYUO VIKUU-PROF MKENDA.

 

Prof. Adolf Faustine Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia

Na Mbaruku Yusuph, Matukio Daima APP. 


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Vyuo vikuu havipimwi kwa wingi wa wanafunzi na mapato badala yake tafiti inazofanya  zenye kuleta gunduzi, kukuza maarifa na ujuzi katika jamii.


Hayo yamebainishwa na Prof. Mkenda Jijini Dodoma wakati akizindua Baraza jipya la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na kutoa wito kwa Vyuo vikuu kuzingatia ufanyaji wa tafiti zenye tija nchini ili kuchochea ushindani katika gunduzi mbalimbali ndani na nje ya nchi.


“Vyuo vikuu havipimwi kwa wingi wa wanafunzi na wingi wa mapato, kuna vipengele vingi vya upimaji ubora wa elimu ya chuo kikuu mojawapo ni ufanyaji wa tafiti. Lazima Chuo Kikuu kiwe chemchemi ya kuvumbua na kutafuta majibu ya changamoto za wananchi kwa kufanya tafiti," amesema Prof. Mkenda 


Ameongeza  kuwa tafiti zinazofanywa na vyuo vyetu ni vyema zikashindanishwa kimataifa ili ziweze kuwa na viwango vya ubora zaidi katika nyanja za kimataifa ili kuvifanya vyuo vyetu viwe na uwezo wa kufanya kazi na watu wa mataifa mbalimbali duniani.


"Hivi karibuni Wizara imetoa tuzo na fedha kwa watafiti ambao wamechapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida ya kimataifa kama motisha lakini pia kuwafanya watafiti wa Tanzania kushindana kimataifa, Niwapongeze OUT kwa kazi nzuri ya kuendelea kuzalisha wataalamu na  kufanya tafiti, mhadhiri mmoja kutoka chuo hiki amepata tuzo hongereni,"amesema Prof. Mkenda 


Amesema Chuo Kikuu ni mahali pa kuzalisha wataalamu na wabobezi ambao wakitoka wanakwenda kufanya kazi za kutoa huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali.


Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Joseph Kuzilwa, amemhakikishia Waziri Mkenda kuwa baraza jipya lililoteuliwa ni la watu wenye taaluma na ujuzi wa kutosha kuweza kusogeza ambele gurudumu la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.


Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema baraza hili jipya limepata fursa ya mafunzo ya siku tatu ambapo wawezeshaji watatoa mada mbalimbali zitakazowajengea  wajumbe uwezo zaidi ili waweze  kutimiza wajibu wao vizuri na kwa ufanisi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI