![]() |
Filemon Makungu; Kamanda wa polisi mkoa Kigoma |
Na Fadhili Abdallah, Kigoma
Watu watatu wakazi wa kijiji cha Kazuramimba wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wamefariki huku polisi wawili wakijeruhiwa kufuatia vurugu kubwa zilizotokea kijijini hapo zikihusiana na vitendo vinavyoendelea mkoani Kigoma vya kutoa uchawi maarufu Kamchape.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa tukio hilo lilitokea wiki iliyopita na haijabainika hadi sasa sababu za vifo vya wananchi hao na kwamba uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea.
Kufuatia hali hiyo alisema kuwa wananchi walikaidi agizo hilo na siku iliyofuata waliamua kuendelea na vitendo vya kutoa uchawi kwenye nyumba za watu huku wakiwanyoa vipara wananchi ambao wanadaiwa uchawi kutolewa kwenye nyumba zao sambamba na kuharibu nyumba hizo.
Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa polisi walipopata habari za vurugu hizo walifika kijijini hapo kuzuia vurugu hizo ambapo wananchi hao walifunga barabara kuu ya Kigoma Tabora inayopita kijijini hapo kwa kuweka magogo na kuwasha moto ili kuzuia polisi na vyombo vya usalama wasiweze kufika kwa urahisi kwenye maeneo wanayofanya matukio hayo.
Ili kudhibiti hali hiyo Kamanda Makungu alisema kuwa polisi walitoa vizuizi hivyo na kuanza kukamata watu ambapo vurugu kubwa zilitokea na kusababisha raia watatu kuuawa, polisi wawili kujeruhiwa, gari mbili za polisi na uhamiaji kuvunjwa vioo na kituo cha polisi kazuramimba kushambuliwa kwa mawe na kuharibiwa.
Hadi sasa watu 49 wamekamatwa kutokana na tuhuma za kuhusika na vurugu hizo wakiwemo raia wa Burundi 15.
Mwisho.
0 Comments