Na Fadhili Abdallah,Kigoma
mikutano na makongamano yanayofanywa na Benki ya NMB kwa kukutana na wateja wao imekuwa na msaada mkubwa katika kupunguza changamoto ya utoaji huduma kwa wateja wao hasa masuala ya mikopo na huduma mbalimbali za bima.
Kaimu Meneja wa kanda ya Magharibi wa benki ya NMB, Gadiel Sawe alisema hayo akizungumza na wanachama wa klabu ya biashara ya benki hiyo Mjini Kigoma katika semina ambapo maafisa wa benki hiyo na wataalam wa fedha kutoka taasisi mbalimbali nchini walikuwa wakitoa mada kuhusu namna ya kufanya biashara yenye tija na namna ya kuepuka changamoto zinapotokea.
Sawe alisema kuwa mikutano hiyo imesaidia kuongeza matumizi ya huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo huduma ya NMB mkononi, kuongeza uwezo wa wateja kuandika michanganuo ya miradi wanapoomba mikopo lakini pia kupata ufafanuzi mbalimbali kuhusu changamoto ya mikopo inapotokea na kupata masuluhisho.
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya Magharibi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya kusaidia sekta binafsi kwenye masuala ya kilimo (PASS TRUST TZ),Hadija Seif alisema kuwa uandishi wa michanganuo ya biashara kwa ajili ya kuomba fedha za kuanzisha biashara au kuomba mikopo kwenye taasisi za fedha imekuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wengi hivyo mikutano na semina hizo zinazofanywa na NMB na taasisi nyingine za fedha zimesaidia kupunguza changamoto hiyo.
Hadija alisema kuwa wafanyabiashara wanaohudhuria mikutano hiyo wamekuwa wakipata miongozo na kuuliza maswali mbalimbali ambayo yamewajenga na kuwafanya kuondokana na changamoto kubwa katika maandiko ya kuomba mikopo lakini pia usimamizi wenye tija wa matumizi ya fedha ambazo wamechukua mikopo kwa ajili ya kuinua biashara zao.
Wakizungumzia semina,makongamano na mikutano wanayofanya na viongozi wa benki na taasisi za fedha Mwenyekiti wa klabu ya wafanyabiashara Kigoma, Aloyce Ntibilaba amesema kuwa yamekuwa na mchango mkubwa katika kupata masuluhisho zinapotokea changamoto kwenye biashara zao Sambamba na kuzifanya biashara hizo kukua.
0 Comments