Na MATUKIO DAIMA APP ,BUKOBA
Zaidi ya nyumba 150 na vyumba vya madarasa 20 vimeezuliwa na upepo katika kata Karambi wilayani Muleba mkoani Kagera, baada ya kunyesha mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali, Oktoba 16 mwaka huu, majira ya asubuhi.
Aidha kufuatia upepo huo, mashamba ya wananchi wa kata hiyo pia yameathiriwa.
Wakizungumza baada ya kutokea kwa tukio hilo, baadhi ya wananchi akiwemo Titus Maghembe, wameiomba serikali kuwasaidia kupata mahala pa kulala na chakula.
Naye Gervaz Marwa mwanafunzi wa shule ya sekondari Karambi, ameiomba serikali na wadau wengine kuwasaidia kukarabati vyumba vya madarasa vilivyoezuliwa na upepo huo, ili kuwezesha wanafunzi kuendelea na masomo, hasa wa kidato cha pili na cha nne, ambao wanakaribia kuanza mitihani yao ya taifa.
Mganga mkuu wa mkoa wa Kagera dk. Issesanda Kaniki amesema kuwa hakuna taarifa ya kifo na kwamba baadhi ya wananchi waliojeruhiwa hali zao zinaendelea vizuri.
Naye katibu tawala wa mkoa wa Kagera Toba Nguvila amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho serikali inaendelea kufanya tathmini, ili kujua hasara iliyotokana na mvua na upepo huo.
Nguvila amesema kuwa tayari halmashauri ya wilaya ya Muleba imekwishatenga fedha shilingi milioni 75, kwa ajili ya kurekebisha miundombinu iliyoharibika.
Meneja wa mamlaka ya hali ya hewa nchini - TMA- mkoa wa Kagera, Stephen Malundo amewaasa wananchi hasa wanaoishi katika maeneo hatarishi ikiwamo mabondeni, kuendelea kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara yanayoweza kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
0 Comments