Na Matukio Daima App,Bukoba
Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera umekabidhi rasmi kwa mkandarasi, mkataba wa ujenzi na uboreshaji wa kituo cha mabasi Bukoba, wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 972.
Mkataba huo wa ujenzi wa awamu ya kwanza ambao unajumuisha ujenzi wa uzio na maeneo ya maegesho ya magari, umekabidhiwa kwa mkandarasi Abemulo Contractor Company Ltd.
Akizungumza katika uzinduzi wa ujenzi wa kituo hicho cha mabasi, mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba Ahmed Njovu, amesema kuwa unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 184 kuanzia sasa.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima amesema kuwa ujenzi na uboreshaji wa kituo hicho, hautaathiri ujenzi wa kituo kipya cha mabasi katika eneo la Kyakailabwa.
"Kituo hiki kikikamilika kitasaidia kupunguza adha iliyopo sasa, lakini pia ujenzi wa kituo kipya cha Kyakaibwa utaendelea, ukikamilika hiki cha katikati ya mji tutaendelea kukitumia na kile kitatumiwa na mabasi makubwa yaendayo mikoani" amesema Sima.
Baadhi ya wafanyabishara waliokuwa wakifanya shughuli zao katika eneo hilo akiwamo Asimwe Kalikawe, wameiomba manispaa hiyo baada ya kituo cha mabasi kukamilika, warejeshwe katika maeneo yao kuendelea na biashara.
Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini Wakili Stephen Byabato, amewahakikishia wafanyabiashara waliohamishwa katika eneo hilo kupisha ujenzi huo, kuwa mradi utakapokamilika watarejeshwa katika maeneo yao.
"Wale wote waliokuwa wakiendelea na biashara hapa, ujenzi utakapokamilika watarejeshwa, maana tunawatambua, kama kuna ambao walikuwa wamelipa kodi zao halafu wakaondolewa, watakaporejea kodi zao zitahesabiwa upya" amesema Wakili Byabato.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa manispaa hiyo, kituo hicho kitajengwa kwa awami mbili, ambapo awamu ya pili itakayogharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili, itaanza mkandarasi atapopatikana.
0 Comments