Na Pamela Mollel - Matukio Daima App, Mkomazi.
Kutokana na kuanzishwa kwa miradi ya wanyama adimu ya Mbwamwitu na Faru weusi katika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, wageni wanaelezwa kuongezeka kwa asilimia 100 katika kipindi cha mwaka 2022/2023 katika hifadhi ya Mkomazi jambo ambalo limechangia ongezeko la mapato
Hayo yamebainishwa na Mhifadhi Mkuu anaesimamia kitengo cha Utalii Happyness Kiemi wakati akielezea mafanikio waliyoyapata kwa waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo hivi karibuni ambapo amesema hayo yametokana na uhamasishwaji uliyofanywa na hifadhi kutokana na kuwepo kwa vivutio hivyo adimu
Kiemi ameeleza kuwa bado wana matarajio ya kuongezeka kwa wageni hususan wageni wa ndani na ongezeko hilo pia limetokana na uwepo wa filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa na Mh.Rais.
“Hifadhi yetu bado ina matarajio ya kuwa na ongezeko la wageni hususan wageni wa ndani ambao wanakuja kutazama Faru na Mbwamwitu na katika kipindi cha miaka miwili ijayo tunatarajia wageni kuongezeka zaidi”.Alifafanua Kiemi.
Kwa upande wake Mhifadhi mwandamizi anaesimamia miradi hiyo ya wanyama adimu Emanueli Sisya ameeleza kuwa hifadhi ya Mkomazi ilichanguliwa kama hifadhi ya uzalishaji Mbwa mwitu kutokana na eneo hilo kushabihiana na mazingira wanayoishi mbwa hao
Sisya amefafanua kuwa mradi huo ulianza ukiwa na mbwa mwitu 25 ila kwa sasa wameongezeka na kufikia zaidi ya 300 ambapo huwaachia mbwa hao katika mifumo ya kiiolojia na kwa sasa lengo lao ni kuzalisha na kuwarudisha katika maeneo yao ya asili
“Mbwawitu ni wanyama wanaoishi kimakundi,”Yaani kifamilia hivyo tunawaachia katika makundi tukiangalia mbwamwitu wenye umri unaolingana”.Alifafanua Sisya
Aidha amezitaja faida zinazotokana na mbwamwitu kuwa ni kivutio kikubwa cha utalii hususan kwa wageni ambao wengi wamekuwa wakitembelea hifadhi hiyo kutokana na uwepo wa kivutio hicho cha mbwa mwitu,na hivyo wana mpango wa kuendelea kutanua kwa kujenga boma lingine ili kuwezesha wageni kuendelea kuwaona na utalii kukua
Kwa upande wake Mratibu wa wanyama hao adimu Jackson Lyimo akazitaja Changamoto kubwa wanazokabiliana nazo mbwamwitu kuwa ni pamoja na migongano baina ya wafugaji na wanyama hao kwa kuwa wanawaona kama wanyama waharibifu
Lyimo amefafanua kuwa tangu kuzalishwa kwa mbwamwitu katika hifadhi ya Mkomazi tayari wameachia makundi 15 yenye mbwa zaidi 209 ikiwa ni kurudisha ikolojia ya hifadhi ya Mkomazi kwa kuwarudisha katika hifadhi ambazo zilikuwa na mbwamwitu ila wakatoweka kutokana na sababu mbalimbali
“Mbwa hawa pia wanakutana na changamoto za magonjwa pindi wanapokutana na wanyama wakufugwa lakini pia binadamu ni adui mkubwa wa wanyama hao kwa kuwa wanamuona kama mharibifu”.Alifafanua Lyimo.
Mradi wa mbwa mwitu katika hifadhi ya Mkomazi ulianzishwa mwaka 1995 ukiwa na lengo la kuzalisha mbwa mwitu na kuwarudisha katika maeneo yao ya awali kutokana na kuendelea kutoweka kutokana na sababu mbalimbali
0 Comments