Na Gabriel Kilamlya-Matukio Daima APP, NJOMBE.
Waziri wa ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi Dokta Anjelina Mabula amewashauri Wananchi 56 wenye mgogoro wa ardhi na Kanisa la KKKT dayosisi ya kusini Njombe katika eneo la Lunyanywi kata ya mjimwema kukubali kupokea viwanja 400 kama kifuta jasho ambazo kanisa lilipanga kuwapa ili kuepusha malumbano yaliyopo kwa kuwa kisheria kanisa lina haki zote.
Awali Greyson Chilongoji Katibu mkuu wa KKKT dayosisi ya kusini Njombe baada ya waziri Dokta Mabula kuwasili mkoani Njombe amesema walinunua eneo hilo NJODECO kwa maelekezo ya kutakiwa kulipa fidia ya mali zilizokuwemo na wakafanya hivyo.
Diwani wa kata ya Mjimwema Nestory Mahenge amesema licha ya mgogoro huo kuendelea kuleta shida katika pande zote lakini haoni ustawi wa shughuli za Kanisa zilizowekezwa katika eneo hilo ikiwemo chuo kikuuu na shule.
Kutokana na hoja za pande zote mbili Waziri Mabula ametoa ushauri huo na kufunga mjadala wa mgogoro huo huku akisema ambao hawatoridhika wanayo nafasi ya kwenda mahakamani.
Mbunge wa Jimbo la Njombe mjini Deo Mwanyika amesema mgogoro huo umekuwa na malalamiko mengi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa muda mrefu huku akisema maamuzi ya mwisho ni ya wananchi kwa sasa.
Baadhi ya wawakilishi wa wananchi akiwemo Julius Lupenza, Lucy Kitavile na Mussa Mhagama wamesema tangu mwaka 2002 mgogoro ulipoanza hakukuwapo na maridhiano mpaka mwaka 2009 waliposikia Kanisa limepata hati miliki Jambo ambalo liliwaongezea hofu kubwa na hivyo hawajakubaliana na maamuzi wa Waziri na kuahidi kwenda mahakamani.
0 Comments