Na Mbaruku Yusuph, Matukio Daima APP Korogwe.
WANANCHI wa Kijiji cha Makuyuni, kata ya Makuyuni Wilayani Korogwe wamekiomba Chama cha Mapinduzi kushughulikia kero ya maji ambayo imedumu kwa muda mrefu na kupelekea kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.
Wakitoa malalamiko hayo mbele ya Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji hicho Wilayani Korogwe.
Mwenyekiti huyo yupo Wilayani Korogwe ikiwa sehemu ya mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Wilaya zote za Mkoa wa Tanga kwa lengo la kukiimarisha chama hicho,kutembelea miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia njia sahihi ya ufumbuzi.
Wananchi hao waliiomba Serikali kupitia mamlaka zake iwatatulie kero hiyo ya kukosekana kwa huduma hiyo muhimu ya maji.
Amina Kangaulaya mkazi wa Kijiji cha Makuyuni alisema kwenye mkutano huo kuwa wananchi katika maeneo hayo wanakabiliwa na kero ya maji ambapo hawajui hatma ya upatikanaji wa huduma hiyo.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Korogwe William Tupa baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi juu ya kero hiyo alisema Serikali inatekeleza mradi wa maji Kijijini hapo wenye thamani ya zaidi ya shs Bil 1.4 mradi unaolenga kuhudumia Vijiji vya Makuyuni,bombalamu na madumu.
Tupa alisema mradi huo utakuwa na vyanzo viwili vya maji ya mtiririko na kina kirefu na tayari serikali imekwisha nunua mabomba kwa ajili ya kufunga mtandao wa mabomba wenye urefu wa mita 33.
Alisema kuwa tayari Serikali imekwisha jenga tank la lita laki tatu na chanzo cha maji mtiririko kimekwisha karabatiwa na tank la maji la lita 90 limekwisha karabatiwa.
"kazi tunayoendelea nayo sasa ni uchimbaji wa mitaro na kufunga mabomba hayo na matarajio ndani ya miezi mitatu ijayo wananchi watarajie kupata huduma hiyo ya maji"Akisema Tupa.
Tupa alisema mradi huo ulikumbwa na changamoto za malipo toka Serikalini na kupelekea kuchelewa kumalizika kwa wakati ingawa ulitarajiwa kumalizika mwezi July 2022.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa aina mbili aina ya kwanza kwa kutumia mkandarasi zaidi ya Shs Mil 600 na aina ya pili kutumia force Account ambapo Shs Mil 800 zitatumika.
Alisema mkandarasi alipata changamoto ya kucheleweshewa malipo toka Serikalini na kupelekea mradi huo kuchelewa ingawa tayari mkandarasi amekwisha lipwa na kazi zinaendelea.
"Kama alivyosema Mwenyekiti Mkoa wa Tanga atawasiliana na mamlaka zetu za juu kwa ajili ya kusukuma malipo ya mkandarasi ili kazi iendelee"Alisema Meneja huyo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman alisema Chama kinapoahidi lazima kisimamie utekelezaji wake na kuisimamia Serikali na hakitamvumilia mtumishi atakayebainika anatumia vibaya pesa za Serikali kwa maslahi yake binafisi.
0 Comments