Header Ads Widget

WANANCHI KIBOSHO WAISHUKURU SERIKALI KWA FEDHA ZA MAENDELEO.


Na Gift Mongi - Matukio Daima App, Moshi.


WANANCHI katika kijiji cha Kirima kati kata ya Kibosho Kirima jimbo la Moshi Vijijini wamepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 50 kutoka serikali kuu ikiwa ni kuunga mkono jitihada za ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi.


Kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo kinaenda kuleta ahueni kwa wananchi kupata huduma za matibabu kwa ukaribu zaidi hivyo kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo 

Akiwa katika ziara ya kutembelea ujenzi wa zahanati hiyo MBUNGE wa jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na rais Dkt Samia Suluhu Hassan imewaunga mkono wanakijiji hao kwa jitihada walizozionyesha.


Katika ziara yake hiyo, Prof. Ndakidemi alikagua ujenzi wa ofisi ya kijiji cha Boro inayojengwa kwa nguvu za wananchi ambapo pia ofisi hiyo ya kijiji tayari imeezekwa na  bado inahitaji kiasi cha shilingi milioni tatu kukamilika. 

Mbunge  aliambatana na viongozi mbalimbali wa chama kutoka wilaya ya Moshi Vijijini wakiongozwa na  Ramadhani Mahanyu ambaye ni katibu wa CCM wilaya ya Moshi Vijijini, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Kata na wataalamu kutoka halmashauri.  


Akiongea baada ya kukagua ujenzi wa zahanati, Prof. Ndakidemi aliwapongeza viongozi wa kata na Vijiji pamoja na wananchi kwa hatua nzuri waliyofikia.


'Hakika mmefanya jambo jema sana katika kujiletea maendeleo na sii kusubiria kila kitu kutoka serikalini na nyie mtakuwa ni mfano wa kuigwa sasa' anasema

Pia aliwaomba wananchi na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kujitolea katika michango mbalimbali ya kimaendeleo ili kufanikisha shughuli za ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa kusaidiana na  serikali.


Katika hatua nyingine Prof Ndakidemi aligawa miche ya kisasa ya migomba na kahawa kwa kuikabidhi kwa viongozi wa vijiji vya Kirima Juu, Kirima Kati na Boro ukiwa ni mwendelezo wa kulima mazao yenye tija na kumkwamua mkulima.


Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Kibosho Kirima, Diwani wa kata hiyo Mhe Inyasi Stoki alisema kuwa jitihada za serikali yao  kuwaletea maendeleo zimeanza kuonekana kwa vitendo kwani kuna miradi mingi inatekelezwa kwa kasi kubwa katika kata yake ikiwemo ujenzi wa madarasa, ghala la kukusanya mazao, barabara, miradi ya maji na kuunganishiwa umeme.


Akikamilisha ziara yake katika Kata ya Kibosho Kirimama Prof Ndakidemi alihutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi katika kijiji cha Boro. 


Aidha aliwafafanulia wananchi miradi mingi ya maendeleo iliyotekelezwa kwenye kata yao katika sekta mbalimbali ambapo zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zimetumika.


Mbunge alimshukuru  Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kata ya Kibosho Kirima fedha za miradi ya maendeleo kama walivyoomba.


Mbunge aliwahakikishia wananchi kuwa katika bajeti ya 2023/2024, wananchi wataendelea kunufaika na fedha kutoka serikalini ambapo miradi itatekelezwa katika sekta za maji, miundombinu ya  barabara, elimu, afya, kilimo na ustawi wa jamii.


Wakieleza kero zao, wananchi walilalamika kuwa wakati wa ukarabati wa barabara ya Boro - Sangiti - KNCU, TARURA hawakuweka Calvats kwenye maeneo nyeti ambapo imesababisha uharibifu mkubwa kwenye njia za mifereji ya asili ambayo ilikuwa inapeleka maji kwenye mashamba ya kahawa, migomba na mbogamboga kwa wakulima.


Mbunge aliiomba ofisi za kijiji wasajili matatizo hayo kikamilifu ili yapelekwe TARURA kwani kwenye mkutano huo hapakuwa na mwakilishi kutoka TARURA.


Kero ingine iliyolalamikiwa ni ile ya kukosekana eneo la kujenga machinjio ya kisasa katika Tarafa ya Kibosho ambapo pia alishauri viongozi husika wawasilishe maombi kwenye vyama vya ushirika ili wanachama waridhie kutoa maeneo ya kujenga machinjio na miundombinu mbalimbali inayogusa maisha yao kwa manufaa ya wananchi wote.


Baadhi ya wananchi waliotoa kero zao walilalamika kuhusu upotevu wa mbao ambazo zilipasuliwa kwa ajili ya matumizi ya kutengezeza madawati katika shule ya Sekondari ya Masoka, lakini zikachukuliwa kinyume na matumizi yaliyokusudiwa.


Kero iliyogusa hisia za wananchi wengi ni ile ya kitendo cha ubakaji wa mtoto wa shule ya msingi uliotokea katika kijiji cha Boro siku za karibuni ambapo wananchi walilalamika kuwa mtuhumiwa ameonekana uraiani baada ya kupata dhamana huko polisi. Akijibu kero hiyo, mwakilishi wa Serikali kutoka dawati la jinsia alisema kuwa ubakaji ni kosa lakini sheria za nchi zimetoa fursa ya dhamana baada ya kukidhi masharti yaliyowekwa.


Akihitimisha mkutano wake, Mbunge Ndakidemi aliwaahidi wananchi wa Kata ya Kibosho Kirima kuwa, atatoa mchango wake katika shughuli yoyote ya maendeleo ambayo ni  kipaumbele kwao. 


Akiongea katika mkutano huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhani Mahanyu alimpongeza Rais Samia kwa namna anavyoendelea kuiongoza nchi na kutafsiri kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 –2025. Pia alimshukuru mbunge na diwani wa Kata ya Kibosho Kirima kwa jinsi wanavyotoa huduma kwa wananchi, na kuwaletea maendeleo. 


 Aliwaomba wananchi waendelee kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi kwani wamejionea maendeleo yaliyopatikana kwa kipindi kifupi.


Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliohudhuria katika mkutano huo, Mzee Celestine Massawe alimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo katika kata yao. 


Vilevile alimshukuru Mbunge wao Prof. Ndakidemi kwa jinzi ambavyo anawapigania wananchi na kuwaunga mkono katika kuwaletea maendeleo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI