Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Mobhare Matinyi, amekabidhi Bendera ya Taifa vijana 7 kuzunguka mikoa 16 kutangaza kazi alizofanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wilayani Temeke.
Akiwakabidhi bendera ofisini kwake, DC Matinyi alizitaja baadhi ya kazi zilizofanywa wilayani Temeke mwaka 2022/23 na thamani ya fedha zilizotolewa na Rais Samia kuwa ni pamoja na miradi ya afya sh. bilioni6.1, elimu ya msingi sh. bilioni 7.6, elimu ya sekondari sh. bilioni 10, maji sh. bilioni 15.5, umeme sh. bilioni 61.6 na barabara sh. bilioni 43.7.
Amesema Vijana hao Wazalendo waliondoka Dar es Salaam leo asubuhi kuanza matembezi katika mikoa 16 kuzitangaza kazi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alisema kwa ujumla wilaya ya Temeke ilipatiwa na Rais Samia zaidi sh. bilioni 152 katika kipindi hicho kutokana na wingi wa wakaazi wake ambao wanafikia milioni 1.35 na nia yake ya kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Aliwaambia vijana hao kuwa katika kilomita 3,624 wanazotarajia kutembea kwa miguu watakutana na ushahidi lukuki wa kazi za Rais Samia.
Vijana hao saba wanaoongozwa na Abihudi Maugo wanatarajiwa kuhitimisha matembezi yao mkoani Manyara wakati wa sherehe za kuuzima mwenge hapo Oktoba 14, 2023.
Vijana wengine ni Sophia Kooni, Beatrice Masanja, Shabani Juma, Jesca Giribert, Flora Erenest na Paul Mkinga. Hii ni mara ya nane kwa vijana wa Temeke kufanya matembezi nchini kuunga mkono matukio au dhima tofauti.
0 Comments