Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa wilaya Kigoma Salum Kalli amepiga marufuku vitendo vya viongozi wa vijiji na wananchi wa kata ya Bitale Halmashauri ya wilaya Kigoma kuendesha vitendo vya kufichua wachawi kwa kutumia waganga wa kienyeji maarufu kama Lambalamba.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Bitale Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa hakuna mahali popote katika wilaya hiyo ambapo ataruhusu vitendo hivyo kufanyika na kwamba watakaokamatwa wanafanya vitendo hivyo watahesabika kuwa ni wahalifu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania serikali haimini masuala ya uchawi na kwa wilaya hiyo akiwa msimamizi wa katiba hataruhusu jambo ambalo limekuwa likileta taharuki kubwa kwenye jamii na kuvunja amani.
Taarifa kutoka eneo hilo zinabainisha kuwa wananchi wamekuwa wakishabikia jambo hilo kwa kuwapokea na kuwahifadhi waganga hao wa kienyeji ili kuwafichua wachawi lakini pia wamekuwa wakipingana na viongozi wa dini wanaotoa mahubiri kupinga jambo hilo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita waumini wa madhehebu yote wamekuwa wakitoka msikitini na kanisani viongozi wanapoongelea na kukemea kuhusu swala hilo.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa wilaya akiwa ameongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya alisema kuwa mkutano huo ni wa amani na kupiga marufuku matukio hayo na kutaka waganga walioleta waondoke mara moja na vinginevyo atachukua hatua kulingana na sheria na taratibu za nchi.
Hata hivyo kauli hiyo ya Mkuu wa wilaya ilipokea tofauti na wananchi hao ambao walianza kuzomea na kumtaka Mkuu huyo wa wilaya aondoke huku wakieleza kuwa hawataacha kutekeleza jambo lao.
0 Comments