Rais wa Niger Mohamed Bazoum ametoa ujumbe wa kuonesha ukaidi kwenye Twitter baada ya wanajeshi kutangaza mapinduzi usiku kucha katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Matatizo yalianza mapema Jumatano wakati wanajeshi kutoka kwa walinzi wa rais walipomchukua mateka.
Waziri wake wa mambo ya nje amesema mapinduzi hayo hayaungwi mkono na jeshi zima, lakini mkuu wa jeshi sasa amesema anaunga mkono utawala wa kijeshi. Bw Bazoum ni mshirika mkuu wa Magharibi katika vita dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu.
Marekani na Ufaransa zote zina kambi za kijeshi katika nchi hiyo yenye utajiri wa madini ya uranium na zimelaani mapinduzi hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alimpigia simu Bw Bazoum akiahidi "uungwaji mkono usioyumba" wa Marekani na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wametaka rais huyo aachiliwe mara moja.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 64, ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Niger miaka miwili iliyopita, aliandika kwenye mtandao wa Twitter siku ya Alhamisi asubuhi na kusema: "Mafanikio yaliyopatikana kwa bidii yatalindwa. Wananchi wote wa Niger wanaopenda demokrasia na uhuru watashuhudia hilo."
Mji mkuu, Niamey, kwa sasa hauna watu, lakini hii ni kwa sababu mvua imekuwa ikinyesha asubuhi yote. Hata maandamano yaliyopangwa na wanaounga mkono mapinduzi hayajafanyika. Lakini watu nchini Niger wamegawanyika vikali kuhusu mabadiliko ya matukio.
Pichani: Bendera ya Urusi ilikuwa ikionyeshwa wakati wa maandamano ya kuunga mkono mapinduzi yaliyofanyika baada ya mvua kunyesha asubuhi.
Wengine wameshtuka na kufadhaika na ilipokuwa ikiendelea siku ya Jumatano, mamia ya wafuasi wa rais walikaidi wanajeshi hao kwenda mitaani na kuwataka wanajeshi kurejea kambini. Walitawanyika baada ya risasi kurushwa kama onyo - milio ya risasi pekee iliyosikika katika mapinduzi haya ya mamlaka bila kumwaga damu.
Wamesema hawatakubali mapinduzi hayo lakini haijabainika watayapinga vipi. Hawajaitisha maandamano yoyote mitaani kwa wakati huu.
Wengine wamefurahishwa na hatua za jeshi, wakishutumu chama tawala kilichoondolewa madarakani kwa ufisadi na kutofanya vya kutosha kuboresha hali ya usalama na kumaliza uasi wa muda mrefu wa wanajihadi.
Nchi mbili jirani, Mali na Burkina Faso, zimekumbwa na mapinduzi yaliyochochewa na maasi ya wanajihadi katika miaka ya hivi karibuni.
Katika nchi zote mbili viongozi hao wapya wa kijeshi wamesogea karibu na Urusi baada ya kutofautiana na Ufaransa, mkoloni wa zamani, ambayo pia ilitawala Niger zamani.
0 Comments