Na Lilian Kasenene, Morogoro
Habari na Matukio App
MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)mkoa wa Morogoro, Pilly Mwakasege, amewataka wanahabari kuchukua nafasi yao na kuwa mstari wa mbele katika kupinga na kuzuia vitendo vya rushwa, hasa katika kipindi hiki cha kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mwakasege alisema hayo wakati mafunzo kwa Waandishi wa Habari mkoa wa Morogoro yanayohusu Sheria na kanuni za kukabiliana na Rushwa kuelekea uchaguzi mkuu 2025.
Mwakasege alisema kuwa waandishi wa habari wana nafasi pekee ya kuhamasisha jamii kuchukia rushwa na kutoishiriki katika maeneo yote ya maisha yao, ikiwa ni pamoja na kwenye mchakato wa kisiasa.
Aliwataka wanahabari kuhakikisha wanafichua na kuripoti vitendo vyote vya rushwa ambavyo vinafanyika siri au hadharani katika mikutano ya kisiasa, ugawaji wa vyeo au maeneo mengine yanayohusiana na uchaguzi.
Alisema rushwa hupelekea uchaguzi usio huru na wa haki, na hivyo ni lazima wanahabari watumie vipindi vyao, makala na taarifa mbalimbali kuelimisha wananchi juu ya haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka bila kununuliwa kwa rushwa.
Kwa kuongezea, Mwakasege alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya strategia ya TAKUKURU kuwashirikisha wadau wote katika mapambano ya rushwa, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari ambavyo vinabebwa kama dira ya jamii.
Kwa upande wake Naibu mkuu wa Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Morogoro Christopher Mwakajinga alisema kuwa wanahabari ni sauti kwa wasio na sauti.
Mwakajinga alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mpango mikakati wa TAKUKURU kuwashirikisha wadau wote katika mapambano ya rushwa, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari ambavyo vinabebwa kama dira ya jamii.
Aliwashauri wanahabari waangalie changamoto zilizopo kwenye maeneo yao badala ya zile za kitaifa kuzipa kipaumbele hususani madiwani na kuacha kuwadharau kwani wao ndio wasimamizi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri.
Mtoa mada katika mafunzo hayo Herry Mwankusye alisema uelewa wa wananchi kuhusu Rushwa na vita dhidi yake umekuwa ukiongezeka na hivyo kuwapa hamasa kushiriki zaidi katika mapambano dhidi ya Rushwa.
Mwankusye alisema nidhamu kwa watumishi wa umma imeendele kuongezeka kwa kuwatumikia vizuri wananchi badala ya kujali maslahi yao binafsi.
"Thamani ya fedha katika miradi ya maendeleo imekuwa ikiongezeka na Tanzania imekuwa ikipanda juu katika orodha ya nchi zinazofanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa,"
Aidha alisema kuwa huo ni uthibitisho kuwa Rushwa unapungua nchini na kwamba maoni ya wananchi kupitia tafiti mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinaonyesha kuwa Rushwa unapungua nchini.
Mwisho.
0 Comments