Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAZIRI wa ujenzi na uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa uboreshaji mkubwa uliofanywa kwenye bandari ya Kibirizi mjini Kigoma itaongeza maradufu usafirishaji wa shehena na abiria kwenye nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kupitia bandari hiyo.
Waziri Mbarawa alisema hayo alipofanya ziara kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati la kuegeshea boti kwenye bandari hiyo ya Kibirizi na kwamba mradi huo unalenga kuifanya bandari hiyo kuwa na tija kubwa.
Mbarawa alisema kuwa nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zinazotumia bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kupitisha shehena zao kutoka nje ya nchi lakini pia zimekuwa zikitumia bandari za mkoa Kigoma kupeleka bidhaa na shehena zo katika nchi hizo.
Katika kuonyesha uwepo wa ufanisi mkubwa wa uboreshaji huo Waziri huyo wa ujenzi na uchukuzi alisema kuwa kuboreshwa kwa bandari za ziwa Tanganyika kunalenga kuongeza spidi
kupakia na kupakua mizigo kutokana na mpango wa serikali wa uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa reli ya kisasa na miundo mbinu ya barabara ambavyo zitafanya kuwepo na usafirishaji mkubwa wa shehena kupitia bandari za ziwa Tanganyika.
Akizungumza katika ziara hiyo Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa bandari, Mhandisi Juma Kijavara alisema kuwa uboreshaji wa bandari za mkoa Kigoma utaiwezesha mamlaka hiyo kuongeza mapato yake kwa kiasi kikubwa kutoka kiasi cha shilingi Bilioni nane kilichokusanywa mwaka wa fedha uliomalizika.
Kijavara alisema kuwa bandari za ziwa Tanganyika ndiyo uti wa mgongo wa usafirishaji wa shehena wa bandari ya Dar es Salaam ambapo asilimia 96 ya shehena hizo zinaenda nchi za ukanda wa maziwa makuu Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo huku kukiwa na ongezeko kubwa la mizigo na abiria kupitia bandari hizo.
Awali Meneja wa mradi huo, Elly Dismass Mtaki kutoka TPA alisema kuwa mradi wa uboreshaji wa bandari za Kibirizi, Ujiji na jengo la Utawala katika bandari ya Kigoma unaogharimu shilingi Bilioni 32 umefikia asilimia 83 ambapo utekelezaji wa mradi huo unahusisha uboreshaji wa bandari ya Kibirizi, bandari ya Ujiji na jengo la Utawala la mamlaka ya bandari Kigoma.
0 Comments