Polisi mkoa wa Pwani wanamsaka Bw Elewa Mahali (53) mkazi wa Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kumchoma moto na kumjeruhi mwanamke ambaye alikuwa mke wake.
Imeelezwa kuwa mtuhumiwa alimchoma mwanamke huyo Bi Dorisi Ogiro (40) anayeishi Bungo Wilaya ya Kibaha ambapo alimfuata mwanamke huyo nyumba waliyokuwa wakiishi na kumwagia mafuta na kumchoma moto mikononi na mapajani kisha kukimbia.
Kaimu kamanda wa Polisi mkoani humo ACP Muhudhwari Msuya alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 23 mwaka huu majira ya saa 2 usiku ambapo mtuhumiwa huyo alifanya tukio hilo kwa kinachodhaniwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Kwa upande wake Bi Ogiro alisema kuwa mtuhumiwa amefika nyumbani akiwa na mafuta ambayo alikuwa ameyaweka kwenye chupa ya maji ya kunywa kisha kuanza kuyamwaga mlangoni na kumwagia mkononi na mapajani.
Alisema kuwa baada ya kumwagia ambapo alitaka amwagie kichwani lakini alikwepa na kumwagikiwa mikononi na mapajani kisha akachukua kiberiti na kumchoma hali iliyomfanya ajitahidi kuvua nguo na baada ya kufanikiwa kuuzima moto kisha kuomba msaada.
Aidha alisema kuwa walikuwa na ugomvi ambapo alimtuhumu kuwa na uhusiano na mwanaume mwingine hali iliyosababisha kuwe na ugomvi na mtuhumiwa akataka waachane na mahakama ikawatenganisha Aprili mwaka huu na kutakiwa kugawana mali ikiwemo nyumba hiyo waliyoijenga kwa pamoja.
0 Comments