Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Baada ya Halmashauri ya mji wa Njombe hapo mei 25 mwaka huu kuwafungia milango ya biashara baadhi ya wafanyabiashara waliopanga katika soko kuu kwa madai ya kushindwa kulipa fedha za pango kwa miezi kadhaa sasa,Baadhi ya wafanyabiashara hao wamelalamikia hatua ya serikali kushindwa kutatua kero zinazowakabili yakiwemo madai ya kuwa na wasiwasi na mfumo unaotumika kukusanya fedha unaotoa taarifa tofauti na kumbukumbu wanazozihifadhi.
Wakizungumza katika mkutano huo uliolenga kuwasilisha kero zao kwenye mamlaka za juu baadhi ya wafanyabiashara hao akiwemo Bahati Mchapi,Richard Mtungi na Angel Upete wanasema kwa muda mrefu kero zao zimeshindwa kutatuliwa katika ngazi ya halmashauri,Wilaya na hata mkoa hadi wanapofungiwa milango ya biashara kwani biashara bado ni mbaya ndani ya soko hilo kutokana na eneo walipo.
Aidha wamesema maduka yaliyofunguliwa tofauti na matarajio ambayo yalipaswa kuwa stoo yamekuwa sababu mojawapo ya kuwafanya wao wasifanye biashara kwakua biashara zinafanana.
Diwani wa kata ya Njombe mjini Alatanga Nyagawa amefika katika soko hilo na kusema yeye yupo pamoja nao.
Kutokana na kadhia hiyo ya kufungwa maduka ya wafanyabiashara hao,Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Erasto Mpete amewaomba waendelee na biashara zao wakati wanashughulikia changamoto zao.
Baada ya agizo la mwenyekiti Mpete wafanyabiashara hao wamerejea na kufungua maduka yao wakati wakisubiri malalamiko yao kushughulikiwa.
0 Comments