Na Shomari Binda-Musoma
WATOTO 10,141 wamekusudiwa kufikiwa na huduma ya chanjo mkoani Mara ili kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo surua na polio.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa mkoa wa Mara,Robert Makungu,wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya chanjo mjini hapa.
Amesema watoto hao ni wale waliopo kwenye ratiba ya chanjo lakini pia watawafikia watoto 1766 walio nyuma ya ratiba ya kupata chanjo.
Makungu amesema katika maadhimisho haya ya wiki ya chanjo watafikiwa pia wasichana 15,782 walio na umri chini ya miaka 14 watakaopewa chanjo ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi.
Amesema chanjo zinazotolewa ni zile zinazotolewa wakati wote na ni salama na kuwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha kila mlengwa anapata chanjo.
Katibu Tawala hiyo amesema mtoto ambaye hajapata chanjo yupo kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa kwa kuwa anakuwa hana kinga ya mwili.
" Leo tunafanya uzinduzi lakini zoezi hili tumelianza tangu Aprili 24 na niwahimize wazazi na walezi kuwapeleka watoto zahanati na vituo vya afya ili waweze kupata chanjo na kufokia lengo.
" Nitowe wito pia kwa wakuu wa wilaya,wakurigenzi na viongozi wa Kata kusimamia zoezi hili kwa ufanisi ili liweze kufanikiwa",amesema Makungu.
Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Mara,Omari Gamuya,amesema chanjo zina manufaa makubwa na kwa sasa hata ugonjwa wa Surua umepunguwa na wodi yake imefungwa.
Meya wa manispaa ya Musoma,Patrick Gumbo, amesema wamejipanga vizuri kwenye maeneo yote ya kutolea huduma za afya ili kuweza kutekeleza huduma za chanjo.
0 Comments