Header Ads Widget

MBUNGE ZUENA BUSHIRI AONGOZA HARAMBEE YA MFUKO WA MAENDELEO YA WANAWAKE MANISPAA YA MOSHI MILIONI 6.9 ZAPATIKANA.



NA WILLIUM PAUL, MOSHI.

MBUNGE wa viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri amejitosa kuhamasisha maendeleo kwa wanawake kwa kuongoza harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya mfuko wa maendeleo ya wanawake manispaa ya Moshi.



Katika harambee hiyo jumla ya shilingi 6,962,200 zilipatikana ambapo lengo la mfuko huo ni kuja kuwa benki ya wanawake hapo badae.


Akizungumza katika harambee hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Uhuru park manispaa ya Moshi, Mbunge Zuena alisema kuwa, kwa sasa wanawake ndio watu wanaoshikilia uchumi kutokana na juhudi wanazozifanya katika kujishughulisha na kazi mbalimbali.



"Wakinamama ni jeshi kubwa na tunaweza sio mpaka tuwezeshwe sisi ndio tumeshikilia uchumi hivyo tunapaswa kupambana kuhakikisha tunajiletea maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na kama familia pamoja na kukuza uchumi wa Taifa" alisema Mbunge Zuena.


Mbunge huyo alisema kuwa, mfuko huo utasaidia kukuza kipato cha wanawake manispaa ya Moshi na kuwataka kuutumia vyema ili uweze kukua.



"Nimeona malengo yenu ya kuanzisha mfuko huu ni pindi utakapokuwa uje kuwa benki ya wanawake hili litawezekana pale tutakapokuwa na matumizi sahihi ya fedha pamoja na kuepuka matumizi yasiyo na ulazima" alisema Zuena.


Katika hatua nyingine Mbunge huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwaasa Wakinamama kujijengea tabia ya kuwa karibu na watoto ili kudhibiti vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto.


Alisema kuwa, kwa sasa kumekuwepo na matukio mbalimbali ya ukatili dhidi ya watoto sasa imefika wakati ambapo jamii inapaswa kuungana kwa pamoja kupinga vitendo hivyo.

Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI