Na Fadhili Abdallah,Kigoma
KAMISAA wa Sensa ya watu na makazi nchini Anne Makinda amewataka viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa kutumia takwimu za hesabu za watu na makazi zilizofanyika kwenye zoezi lililofanyika mwaka 2022 kuziingiza kwenye mipango yao ya maendeleo ili ziweze kuleta matokeo ya haraka kwenye utekelezaji wa mipango hiyo.
Makinda alisema hayo akizungumza na viongozi wa Tawala za mikoa na serikali za mitaa katika manispaa ya Kigoma Ujiji kwenye mafunzo ya ya matumizi ya takwimu kwa viongozi hao katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa zoezi hili ambapo kwa sasa zoezi hilo limeingia kwenye hatua ya uchakati, uchambuzi na uhakiki wa takwimu hizo.
Alisema kuwa kuna mahusiano makubwa ya upangaji wa mipango ya maendeleo na takwimu za watu na makazi zilizopo kwenye eneo husika ambapo mipango hiyo itawezesha rasilimali mbalimbali kutumika wakati utekelezaji kulingana na idadi ya watu na makazi ya eneo husika.
Alisema kuwa wakuu wa idara wa halmashauri, watendaji wa kata,madiwani na watendaji na viongozi kwenye mitaa wanapaswa kuwa na takwimu hizo mpya za sense ambazo zinapaswa kutumika kwenye shughuli zao mbalimbali ikiwemo kuibua na kupanga mipango ya maendeleo badala ya takwimu hizo kukaa kwenye makabati na kutumia takwimu wanazojua wao.
Akieleza hali ya zoezi la sensa ya watu na makazi lililofanyika alisema kuwa mkoa Kigoma umeonekana kwa sasa kuwa na ongezeko dogo la idadi ya watu ikiwa ni asilimia 1.5 ukilinganisha na sensa ya mwisho ya mwaka 2012 ambao mkoa huo ulikuwa na ongezeko la watu kwa asilimia 2.4.
Akitaja sababu ya ongezeko hilo dogo kuwa linasababishwa na kuimarika kwa amani nchini Burundi ambako kumefanya kuwa na kupungua kwa wahamiaji haramu wanaoingia nchini au wakimbizi wanaotoroka makambini na kuishi uraiani.
Kwa sasa mkoa Kigoma una wakazi milioni 2.4 kwa mujibu wa matokeo ya sensa hii iliyofanyika ukilinganisha na watu milioni 2.1 waliokuwepo kwenye sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk.Albina Chuwa alisema kuwa mamlaka za serikali za mitaa ndiko kwenye chimbuko la uibuaji na upangaji wa mipango ya maendeleo ya wananchi hivyo kuwepo na kutumiwa kwa takwimu hizo kwenye maeneo yao ni jambo kubwa ambalo linatimiza dhamira ya zoezi la sensa ya watu na makazi.
Alisema kuwa ni lazima madiwani,wenyeviti wa mitaa na vijiji, watendaji wa vijini,mitaa na kata wanapaswa kutembea na takwimu hizo popote wanapokuwa ili iweze rahisi kwao katika kuanza kuibua,kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
Naye Mkuu wa wilaya Buhigwe, Michael Ngayalina akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa mkoa umejipanga kutekeleza program na mipango ya maendeleo kulingana na takwimu ambazo zimekusanywa kwenye zoezi la sensa.
Alisema kuwa takwimu hizo kuwekwa kwenye mipango kutajibu kwa haraka changamoto zilizopo kwenye maisha ya kila siku ya wananchi na kuhakikisha wanapata huduma bora na zinazostahiki kwa wakati zenye kuzingatia mahitaji halisi kulinganisha na idadi yao, jinsi yao na mahitaji maalum ya makundi ya jamii kuzingatia mazingira wanayoishi.
0 Comments