Header Ads Widget

UKEKETAJI KWA WANAWAKE NA WATOTO WAKIKE NCHINI BADO NI TATIZO

 


Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amesema takwimu zinaonyesha kuwa ukeketaji nchini bado ni tatizo hali inayotokana na baadhi ya jamii zetu kuendelea kukumbatia mila na desturi zenye madhara na kuwadhalilisha watoto wa kike.


 Akiongea jana Februari 2 ,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa hukusu siku ya Kimataifa ya kupinga Ukeketaji dhidi ya Wanawake na Watoto wa kike Duniani ambapo amesema Madhara hayo ni pamoja na kupoteza damu nyingi na kusababisha vifo, maambukizi ya VVU/UKIMWI na kusababisha matatizo wakati wa kujifungua. 


Amesema Watoto wakati wa kukeketwa hushindwa kuhudhuria shule kwenye vipindi kwa muda mrefu na hivyo kuzorotesha maendeleo yao kielimu.


"Serikali kwa kushirikiana na Wadau inaendelea na jitihada za kukabiliana na vitendo vya ukeketaji kupitia mipango na mikakati iliyowekwa ikiwemo kutunga na kufanya marekebisho ya sheria na sera mbalimbali za nchi," Amesema Dkt Dorothy.


 Aidha amesema ,Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inasisitiza usawa na heshima kwa binadamu wote, kutambua na kuthamini utu wa mtu pamoja na kuhakikisha haki mbele ya sheria.


" Hivyo kutokana na hayo mwaka huu 2023 maadhimisho haya yatafanyika katika ngazi ya Mikoa, kulingana na mazingira yao na kiwango cha hali ya ukeketeji ambapo, Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji Duniani ni “Wanaume na Wavulana; Tushiriki Kupinga Mila na Desturi zenye Madhara ili kutokomeza Ukeketaji,”amesema Dkt Dorothy. 


Ameeleza  Kauli mbiu hiyo inahimiza ushiriki wa wanaume na wavulana katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukeketaji ambayo ni kinyume cha Sheria na kinyume cha haki za binadamu.


 Pia, kaulimbiu inatambua umuhimu wa wanaume na wavulana katika kushawishi  wanawake na watoto wa kike  kutotamani kufanyiwa  ukeketaji. 


"Kwa ajili hiyo mitazamo ya wanaume inatakiwa kubadilika kwanza ndipo jitihada za kupinga ukeketaji zinaweza kufanikiwa," Amesema 


Na kuongeza "Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika ngazi zote kwa kuandaa Mdahalo wa Wadau wanaotekeleza shughuli za kutokomeza ukeketaji nchini pia kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji kwa njia ya mikutano ya hadhara, vikao na maandamano. 


Hata hivyo tarehe 06 Februari, 2003 Baraza la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kufanyika kwa Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike duniani Siku hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 06 Februari. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI