Header Ads Widget

TUTATUMIA SHERIA NA MIONGOZO ILIYOPO KWA WAZAZI WASIOPELEKA WATOTO SHULENI

 



NA HADIJA OMARY  _LINDI......



Wazazi na walezi wa vitongoji, kata na tarafa zote Wilayani  Ruangwa Mkoani Lindi wenye watoto waliofaulu na wanaopaswa kuripoti darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza, na bado wapo majumbani, wametakiwa kuwapeleka mara moja ili kutimiza haki  zao za msingi.



Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi Bw. Hassan  Ngoma  wakati akizungumza na Blogu ya Matukio Daima tarehe 2 Februari 2023 katika mahojiano maalum.



Ngoma amesisitiza kuwa kuanzia tarehe 6 Februari 2023 ofisi yake itaanza kufanya msako mkali wa mtaa kwa mtaa na nyumba kwa nyumba ili kubaini watoto waliofaulu kuingia kidato cha kwanza na wenye umri wa kuanza darasa la kwanza  na bado hawajaripoti shule, na wazazi na walezi wao watachukuliwa hatua kali za kisheria.




Ngoma alisema kuwa kwa sasa wanaendelea kufanya ziara katika kata mbali mbali za Wilaya hiyo ambapo mpaka sasa tayari wameshazungumza na wazazi na walezi katika kata 12 kati ya kata 20 za Wilaya hiyo ambapo matarajio yake ni kwamba mpaka siku ya Jumamosi tarhe 4.2. 2023 atakuwa amekamilisha ziara yake kwa kata 8 zilizosalia.





"Baada ya hapo kitakachofuata ni kutumia vyombo vya sheria ambavyo kuanzia wiki ijayo tutaingiza gari za polisi na mgambo mtaani kwa wale wote ambao wamekaidi na wameshindwa kufikisha watoto shuleni mpaka kufikia Ijumaa tutawakamata, watawekwa kizuizini polisi, watachukuliwa maelezo na kupelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria ".




Ameongeza kuwa, “suala la kumpeleka mtoto shule sio ridhaa kwamba mzazi anaweza kuchagua kuwa mtoto aende au asiende, suala la kumpeleka mtoto shule ni wajibu na ni lazima mtoto umpeleke shule na usipo mpeleka ni kosa kwa mujibu wa sheria hivyo sheria zipo na hatua za kuchukuliwa zipo".



Hata hivyo Ngoma alibainisha kuwa katika maeneo yote waliyopita mpaka sasa, wazazi na walezi wanaonekana kufanya vizuri katika suala la kuwapeleka watoto wao kwenye elimu ya awali na msingi ambapo kwa kiwango kikubwa ingawa bado yapo maeneo machache ambayo watoto hawajaenda shule kwa sababu mbalimbali  huku kwa upande wa Sekondari likiwa bado na changamoto. 




"Katika ziara yangu hiyo ninayopita kila kata miongoni mwa mambo ambayo tunayasisitiza ni uandikishaji wa watoto wa katika darasa ya awali na darasa la kwanza, kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza,  msisitizo wa kupinga mimba na ndoa  za utotoni,  kukagua miradi ya maendeleo,  kuangalia shughuli za wananchi hasa kilimo, kuongea na kusikiliza kero za wananchi" alifafanua Ngoma.




Kwa upande wake akizungumzia hali ya uandikishaji wa wanafunzi kwa madarasa ya awali na la kwanza ofisa elimu awali na msingi Halmashauri ya Ruangwa mwalimu George Mbesigwe alisema mpaka sasa Halmashauri hiyo wamevuka lengo la maoteo ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo mpaka sasa wameshafika asilimia 117 % .




Alisema kwa mwaka wa masomo 2023 Halmashauri hiyo iliotea kuandikisha wanafunzi wa awali 3,367, wavulana 1,664 na wasichana 1,703 ambapo mpaka Februari  2, 2023 tayari wameshaandikisha wanafunzi 4087 ambapo wavulana ni 2068 na wasichana ni 2,019 sawa na asilimia 121%.




Kwa wanafunzi wa darasa la kwanza maoteo yalikuwa 3,403 wasichana 1,674 na wavulana 1,729 ambapo mpaka sasa tayari wameshaandikisha wanafunzi 3,471 wavulana 2,013 na wasichana1,958 sawa na asilimia 117%.




Mbesigwe alisema hali ya uandikishaji kwa mwaka 2023 imeongezeka mara dufu ukilinganisha na mwaka jana ambapo kwa mwezi kama huu wa Februari uandikishaji ulikuwa ni asilimia 75% kwa darasa la kwanza na asilimia 65% kwa awali.



Hata hivyo Mbesigwe alisema zipo sababu mbali mbali zilizopelekea uandikishaji wa wanafunzi hao kupanda ambazo ni pamoja na mabadiliko ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo miaka ya nyuma uandikishaji huo ulikuwa ukifanyika kuanzia Disemba mpaka Machi na sasa unafanyika Oktoba mpaka Disemba.




Sababu nyingine aliyoitaja kupelekea uandikishaji huo kuongezeka ni uboreshwaji wa hali ya miundombinu mashuleni inayowavuti watoto kutamani kusoma na wazazi kupenda kuwapeleka watoto wao shuleni, pamoja na ujenzi wa miundombinu mipya ya madarasa ambayo hayakuwepo.




Naye mwalimu wa darasa la awali Neema Ngonyani katika shule ya msingi Ruangwa  alisema miongoni mwa changamoto wanayokabiliana nayo walimu kwa wanafunzi wanaochelewa kuandikishwa shule ni kushindwa kuwafundisha katika mtiririko unaotakiwa kwani wale walioanza kufika watakuwa mbele zaidi katika ujifunzaji ukilinganisha na mwanafunzi ambae atakuja baadae.




"Kuandikishwa kwa watoto wakati masomo yameshaanza kwetu sisi inakuwa ni changamoto kwa sababu unakuwa huendi nao sawa kwa kuwa wengine wanawahi wanakuja kuandikishwa mwezi wa kwanza wengine mwezi wa pili, kwa hivyo na wewe huwezi ukakaa ukiwasubiri wale ambao hawajaandikishwa, unakuwa tayari umeshaanza kwa sababu mtaala unakutaka uanze hivyo wanaokuja mwezi wa tatu wa pili wanakuwa hawaendi sawa na wewe"  alisema Mwalimu Ngonyani .




Naye mwalimu wa darasa la kwanza Elizabeth Masue katika shule ya msingi Ruangwa alisema kitendo cha wanafunzi kuchelewa kuandikishwa shule kinawafanya walimu kuwa na mrundikano wa majukumu mengi kwa sababu wanatakiwa kutafuta muda wa ziada kuwafundisha wanafunzi waliochelewa ili waende sawa na wanafunzi wengine ambao waliwahi kufika shuleni.





"Mimi ile Januari ninapofungua shule ninakuwa na azimio la kazi kuanzia ile wiki tunayofungulia kama ni ya kwanza  au ya pili kwa hivyo ninavyofungua natakiwa kuwafundisha wale watoto sasa mwingine anakuja mwezi wa pili mwingine wa tatu, lazima atakuwa tofauti na yule aliekuja mwezi wa kwanza hivyo inanilazimu kutafuta muda wa ziada ili kumfundisha yule aliechelewa kufika shule ili awe sawa na wengine vinginevyo nisipofanya hivyo nikitoa mazoezi au mitihani darasani hataweza kufanya vizuri kwa sababu vile vitu hajavisoma".




"Tunashukuru Serikali kwa kusema kwamba uandikishaji uwe kuanzia mwezi Oktoba mpaka Disemba maana tutakapoingia darasani tutaanza moja kwa moja na wanafunzi wote bila changamoto yoyote tofauti na ilivyo hivi sasa kwa sababu unakuta kama nitaanza nao wote kwa pamoja wakiwa darasani ufaulu na upokeaji wao utakuwa ni mzuri"  alifafanua mwalimu Mesue.




Kwa upande wake Bashiru Nangatika mkazi wa Ruangwa aliwashauri wazazi wenzie wa Wilaya hiyo kuwapeleka watoto shuleni kwani urithi wa mtoto kwa maisha ya sasa ni elimu pekee.




"Kwa hali iliyopo kwa sasa hatuna sababu ya kukimbizana na serikali ili kuwapeleka watoto wetu shuleni ifike mahali itoshe tu kusema kwamba serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya madarasa pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi" alisisitiza mzazi huyo.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI