Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Ili kuepukana na migogoro mingi ya ardhi inayosababisha mauaji na hata ukatili mbalimbali Halmashauri ya wilaya ya Njombe imekabidhiwa hati 15 za ardhi yake baada ya kupimwa ikiwa ni mkakati mojawapo wa kurasimisha ardhi katika maeneo yote nchini.
Katika mkutano wa baraza la madiwani wa robo ya pili ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 afisa ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe kwa niaba ya kamishna wa ardhi nchini Bwana Robert Makwenzi amesema hati hizo zitasaidia kuondoa kabisa migogoro ya ardhi pamoja na uvamizi wa maeneo unaofanywa na baadhi ya watu.
Awali mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Valentino Hongoli amesema kukabidhiwa hati hizo 15 za ardhi ni miongoni mwa mikakati ya kuhakikisha mali zote za halmashauri zinalindwa na kila mmoja.
Hata hivyo baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo akiwemo Innocent Gwivaha, Michael Mbanga na Javani Ngumbuke diwani wa Kata ya Ukalawa wamekiri kuwapo kwa migogoro mingi ya ardhi inayosababisha vurugu kwenye baadhi ya maeneo na kwamba kupatikana kwa hati miliki za ardhi kutapunguza changamoto hizo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa anasema hati hizo ni kinga tosha ya uhalali wa mali za halmashauri hiyo kwenye upande wa ardhi huku akiwapongeza kwa kufanikisha kupatikana kwa hati hizo.
Mpango wa serikali ni kuona maeneo yote nchini yanapimwa na kuwa na hati ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kama mikopo,Dhamana,Kuondoa migogoro pamoja na mauaji yanayosababishwa na ardhi.
0 Comments