Header Ads Widget

KAULI YA RAIS DKT. MWINYI YAPONGEZWA NA WADAU WA VYAMA VYA SIASA.

 



NA THABIT MADAI,ZANZIBAR - MATUKIO DAIMA


KUFUATIA kauli ya Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi ya kuwataka Wafanyabiashara nchini Kupunguza Bei za Bidhaa hususani za Vyakula, Wadau wa Vyama vya Siasa wameibuka na kupongeza kauli hiyo na kuwataka Watendaji wa Serikali kuchukua hatua stahiki ili kupunguza mfumuko wa bei  ambao unawaathiri Wananchi.


Aidha, Wadau hao wa vyama vya Siasa wamesema kwamba, Kauli hiyo ya Rais imelenga moja kwa moja kuwapungizia wananchi ukali wa Maisha unaotokana na kupanda kwa bei za Bidhaa kila kukicha.


Akizungumza leo na Waandishi wa Habari leo Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini Ameir Hassan Ameir amesema hali ya Maisha Visiwani humo ipo juu kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa haswa vyakula.


"Bei za Vyakula  Kama vile, Mchele, Mafuta na Mikate imekuwa juu na kila siku  inapanda huku Mamlaka husika zikiwa zipo Kimya wakati Maisha visiwani hapa  yanazidi kuwa magumu," Amesema Ameir Hassan.


Ameongeza kwa kuwaomba Wafanyabiashara kutii agizo la Rais la kuwataka kupunguza bei za Bidhaa ili kupunguza ukali wa maisha kwa Wananchi.


"Tunaelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Tunawaomba sana Wafanyabiashara kutii agizo la Rais ili huyu mwananchi Mnyonge aweze kufinga Mwezi huu bila Tabu ya Aina yoyote pamoja na  kuishi kwa Amani katika Nchi yake," Ameeleza.



Hata hivyo Ameir ameshauri Serikali kuunda Tume Maalum ambayo itachunguza sababu zinazopelekea kupanda hovyo  kwa bidhaa Visiwani humo.



Ameongeza Kuwa, Mamlaka kama vile ZAECA wanapaswa kuchunguza kwa Makini madai ya Wafanyabiashara ya kupandishiwa kodi kwa Bidhaa zinazoingia Nchini.


"Nishauri Serikali kuunda Tume maalumu itakayochunguza kwa kina Sababu za kupanda kwa bei za Bidhaa pamoja na kufanya Operesheni maalum katika Maghala ili kuangalia kama kuna Wafanyabiashara wameficha Bidhaa ili kupandisha bei," Amefafanua.


"Kuna Madai mbele ya wafanyabiashara wameyatoa mbele ya Rais ya kupandishwa kwa Kodi licha ya Serikali kuwapunguzia hivyo niwaombe ZAECA kuchunguzwa kwa kina Mandarini na kuwachukulia hatua wale wote watakao bainika," Ameongeza.


Nae Katibu Mkuu wa Chama cha UPDP Hamadi Ibrahimu amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara Zanzibar  kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuweka bei elekezi kwa Bidhaa za chakula lengo likiwa kukabiliana na Mfumuko wa bei.


"Waziri wa Viwanda na Biashara wakati Saruji imepanda bei ulijitokeza na kuweka bei elekezi kwa sasa Bei za bidhaa za vyakula zinapanda upo kimya hadi Rais anazungumza na Wafanyabiashara, Tunakuomba jitokeze na kuchukua hatua Stahiki," Amesema.


Kwa upande wao Wananchi mbalimbali Visiwani  wameeleza kuwa kupanda kwa bei za Bidhaa kunapelekea hali ya Maisha kuwa ngumu.


Ikumbukwe Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi alikutana na kufanya Mazungumzo na Wafanyabiashara na kuwataka kupungiza bei za Bidhaa ambazo zimepanda mara dufu.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS