Na Gift Mongi MATUKIO DAIMA APP,MOSHI
Kwa siku za karibuni kumezuka wimbi la wakulima hususani wa mbogamboga kutumia sumu zenye kemikali katika kuua wadudu wanaoshambulia mazao hayo bila kuwepo kwa tahadhari za kina.
Utumiaji wa sumu hizo au viwatilifu umekuwa ukifanywa bila uwepo wa ushauri wa kitaalamu huku mlaji wa mwisho akiwa ni mhanga wa mwisho.
Wengi wanaotumia njia hii hufanya kwa lengo la kujipatia faida bila kujali mlaji matokeo yake yatakuwaje pindi anapokula mbogamboga zenye viambata sumu.
Miongoni mwa maradhi ambayo yanapatikana au kutokea pindi mtu au mlaji anapotumia mboga hizo ni pamoja na kupatwa na maradhi ya saratani.
Katika maisha yetu ya kila siku ni ukweli usiyo na shaka kuwa mboga mboga hizi tumekuwa tukizitumia au hata mabaki ya maji yenye viambata hivyo kwani mbogamboga nyingi hulimwa kandokando ya vyanzo vya maji.
Profesa John Shao ambaye ni mtaalamu daktari bingwa wa uchunguzi wa vijidudu na madawa, (Medical Microbiology and Immunology), amesema kuwa watu wengi huwa tumekuwa na utaratibu wa kutopenda kuchukua tahadhari.
'Mambo yameshabadilika kila mtu ni lazima achukue tahadhari ya afya yake lakini vinginevyo maradhi ya saratani yataendelea kuwepo'alisema Prof Shao
Prof Shao anaeleza kuwa walaji wa mboga mboga hawana budi kuchukua tahadhari katïka matumizi ya mboga mboga ambapo hivi sasa hulimwa kwa viambata sumu
Kwa mujibu wa Shao ambaye pia aliwahi kuwa mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya KCMC ya mjini Moshi ni kuwa njia za asili zinatakiwa kutumika katika kupunguza madhara hayo ya saratani.
'Hapa wala sio mbogamboga tu bali hata maji ambayo yapo katika sehemu ambayo viwatilifu hivyo vimepulizwa tayari nayo ni maradhi pia'alisema Shao.
Baadhi ya maradhi hayo ni pamoja nasaratani ya ngozi,saratani ya tumbo na aina nyinginezo ambazo hujitokeza kutokana na wingi wa sumu za mlaji alivyotumia.
Chikira Mcharo ni afisa kilimo halmashauri ya Moshi ambapo alisema katika eneo lake kumekuwepo na wakulima wa namna hiyo ila kinachofanyika ni utoaji wa elimu.
Amesema kuwa wakulima walio wengi huwa na tabia ya kulima kwa mazoea na hata viwatilifu wanavyotumia havina ushauri wowote wa kitaalamu.
'Mtu analima mbogamboga ila akiona mabadiliko yoyote hukimbilia kununua dawa na kupuliza bila hata kuchukua tahadhari yoyote ile'alisema Mcharo
Alisema kuna baadhi ya maeneo kama Kahe,Chekereni au hata Tpc ambapo tayari wameshapita kutoa elimu kwa wakulima hao ambao hutumia dawa sumu hizo.
Amefafanua kuwa hata dawa nyingine zimekuwa hazieleweki tarehe ya kutengenezwa au hata nchi zilipotoka nalo ni jipya tena na ni changamoto kwa wakulima hao.
Rose Chitundu mama muuza mboga soko la mbogamboga la Manyema katika Manspaa ya Moshi alisema wateja wengi hupenda mboga zilizonawiri na mara nyingi zinakuwa siku si nyingi zimepuliziwa viwatilifu hivyo.
Naye Richard Njau mkazi wa Mwika sokoni kata ya Mwika Kaskazini amesema hali ya matumizi ya vyakula vyenye sumu haipo kwenye mbogamboga peke yake bali ni suala mtambuka na linahitaji tahadhari ya kina.
0 Comments