Na Gift Mongi MATUKIODAIMA App,_Moshi.
Wakulima wameshauriwa kuachana na matumizi ya mbegu zilizobadilishwa vinasaba (GMO) kwa kigezo cha kukabiliana na njaa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyopelekea uhaba wa mvua kwani zinasababisha hasara kubwa kuliko wengi wanavyodhani.
Hata hivyo mbegu hizo mbali nakuwa hazifai kurudishwa tena shambani kama zilivyo zile za asili bado pia zinatajwa kutokuwa na virutubisho vinavyohitajika ambavyo hupatikana katika mazao ya asili.
Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na kilimo hai hapa nchini (FLORESTA) Richard Mhina amesema kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyopo kwa sasa haungi mkono kwa wakulima kukimbilia mbegu zilizobadilishwa vinasaba na badala yake wakulima waendelee kutumia mbegu za asili.
"Siungani na mkulima yoyote anayekimbilia hizi mbegu za kisasa kwani zina hasara kwa mkulima kuliko faida ambayo inaipata kwa kipindi kifupi maana yake wakulima wengi hawajaliona hili"alisema
Mhina amesema kwa mkulima anayetumia mbegu hizo hulazimika kila msimu kwenda kununua mbegu dukani na akiwa hana fedha itamuwia vigumu kuweza kulima tofauti na miaka ya nyuma ambapo mkulima akivuna mazao yake huchagua hapo mbegu nzuri tayari kwa msimu unaofuata lakini hizi za kisasa hazifai.
Amesema ili wakulima waweze kufanikiwa kuondokana na tatizo hilo ni vyema serikali kupitia wizara ya kilimo kuweza kuwekeza katika tafiti ambazo zitakuja na majawabu ya kwanini mbegu za asili zisitumie muda mchache katika kuzalisha na nini kifanyike.
"Uwekezaji huu upo lakini huenda hautoshi ila ukifanyika ndio utabaini ni mbegu zipi zinastahimili ukame lakini pia kuzaa kwa wingi badala ya kuendelea kutumia mbegu za kigeni ambazo zinapoteza zile za asili tulizozizoea wakati wote "alisema
Kwa mujibu wa Mhina ni kuwa A kuendelea kutumia mbegu hizo ni kuongeza umaskini kwa mkulima badala ya kumsaidia ambapo kila baada ya msimu analazimika kutumia kiwango cha fedha ili aweze kupata mbegu nyingine wakati angeweza kuhifadhi kutoka katika mazao aliyovuna.
Mkulima wa mahindi kata ya Kahe Mashariki Emanuel Uronu alisema kilimo cha kutumia mbegu za kisasa ni gharama kwa mkulima japo wakulima wengi hawaangalii gharama walizotumia
Amesema wakulima walio wengi Kwa sasa wamekimbilia katika mbegu hizo kutokana na kuzaa kwa wingi lakini pia kwa muda mfupi jambo ambalo linawalazimisha kila msimu kwenda kununua mbegu mpya ambapo pia zinaweza kukataa kutokana na hali ya hewa.
0 Comments