HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imesema kuwa kamati za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ni njia pekee itakayoondoa hofu ya kukabili magonjwa hayo yanapotokea ndani ya jamii.
Hayo yalisemwa Mlandizi Wilayani Kibaha na Hamad Omary mwakilishi wa mkuu wa Wilaya wakati wa mafunzo ya namna ya kukabili magonjwa ya mlipuko kwa wadau wa afya kwenye Halmashauri hiyo.
Omary alisema kuwa jamii imekuwa na hofu inapokumbwa na magonjwa ya mlipuko hasa wakati wa kupewa kinga au tiba ya magonjwa hayo.
"Mojawapo ni pale ulipotokea ugonjwa COVID-19 ambapo ilipofikia hatua ya utoaji chanjo ya ugonjwa huo kulitokea dhana mbalimbali ambazo zilizua hofu kwa watu kuchanja,"alisema Omary. Kwa upande wake Johnson Mndeme kutoka Wizara ya Afya Idara ya Kinga sehemu ya huduma ya afya alisema kuwa kamati hizo zimeanzishwa ili kutoa elimu juu ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Mndeme amesema kuwa pia itakuwa ikihamasisha juu ya chanjo mbalimbali za kukabiliana na magonjwa ambapo ulipotokea ugonjwa wa COVID-19 jamii ilikuwa haina uelewa wa pamoja juu ya chanjo hivyo kutokea changamoto ya uchanjaji. Naye Ofisa Mawasiliano wa magonjwa ya dharura ambaye ni mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Jaliath Rangi alisema kuwa kamati hizo ni mabalozi kwenye jamii.
0 Comments